Mwl. Christopher Mwakasege - Mambo ya Msingi ya Kutafakari kabla ya kufanya Uamuzi wa Kuoa/Kuolewa.
JAMBO LA KWANZA: Kuoa au kuolewa kunabadilisha uhusiano wako na wazazi wako.
Mwanzo 2:24 anasema, “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili moja”. Ukiangalia (Zaburi 45:10-11) anasema, “Sikia binti utazame (maana yake anazungumza na msichana)... utege sikio lako. Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako na mfalme atautamani uzuri wako, maana ndiye bwana wako naye umsujudie.”
Najua watu wengi sana wanataka waingie kwenye ndoa, waoe au waolewe, lakini uhusiano wao na wazazi wao usibadilike, haiwezekani. Biblia imeweka wazi kabisa, unataka kuoa, mwanamume lazima kwanza aachane na baba yake na mama yake, maana yake kuna mabadiliko. Kuna mabadiliko mahali pakuishi, kuna mabadiliko juu ya mtazamo wako wa kwanza wa maisha yako. Mke wako hawezi kuwa mama yako, na mume wako hawezi kuwa baba yako. Mke wako anakuwa mke wako na si mama yako. Mume wako anakuwa mume wako na si baba yako.
Na kabla hujafikia maamuzi ya namna hiyo, ukiingia kwenye ndoa, ndoa yako itakuwa ngumu. Maana inawezekana unaishi vizuri na wazazi wako, kiasi ambacho maamuzi yako yoyote unayofanya lazima ushirikiane nao, na hiyo ni hatua nzuri kabisa. Lakini ukiishaingia kwenye ndoa, mtu wa kwanza wakushirikiana naye ni mke wako kama umeoa, na ni mume wako kama umeolewa lakini, sio baba yako, sio mama yako.
Na wazazi wengine wasingetaka kuona kwamba unakuwa mbali nao kwa jinsi hii, wanataka waendeleze maamuzi yao na utawala wao waliokuwa nao juu yako mpaka kwenye ndoa yako, haiwezekani. Biblia inakataa. Sasa ukisoma ile Mwanzo unaweza ukafikiri ni wanaume tu wakioa ndio wanatakiwa watoke, waachane na wazazi wao, lakini Zaburi 45:10-11 inatuambia wazi kabisa, inasema, “Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako. Naye Mfalme atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie”.
Sasa haimaanishi usiwasalimie, haimanishi usiwasaidie, lakini ningekuwa nazungumza kwa kiingereza ningekuambia, “your priorities must change” lazima ubadilike jinsi ambavyo unaweka vipaumbele katika watu ulio nao.
Unapoamua kuolewa, wa kwanza sio baba yako wala sio mama yako, wa kwanza ni mume wako baada ya Yesu. Katika mahusiano ya kibinadamu anayekuja pale wa kwanza baada ya Yesu moyoni mwako ni mume wako. Ikiwa hujafikia maamuzi ya namna hii moyoni mwako basi bado hujafikia utayari wa kuolewa. Na ina madhara yake magumu. Maana biblia inasema, kabla hujawasahau watu wako na watu wa nyumba ya baba yako, mume wako hawezi kuutamani uzuri wako, ukitaka autamani uzuri wako lazima uwasahau kwanza watu wa nyumbani kwa wazazi wako.
Sasa kuna tofauti ya kupenda na kutamani. Kabla hujaolewa au kabla hujaoa huruhusiwi kutamani. Lakini ukiisha oa unaruhusiwa kutamani lakini mke wako tu. Ukiishaoa kutamani mke wako ruksa, na biblia imeweka vizuri kabisa, na ukiishaolewa kutamani mume wako ni ruksa. Lakini biblia imeweka utaratibu wa ajabu sana kwamba, ili mume amtamani mke wake, lazima mke wake awasahau kwanza watu wa nyumbani mwa wazazi wake. Hiki ni kigezo kigumu sana.
Ndio maana unaweza ukakuta mtu ana mke mzuri sana lakini hamtamani. Unaweza ukafikiri labda ni kwa kuwa hajajipamba vizuri; lakini hata kama atajipamba, atajikwatua kuanzia asubuhi mpaka jioni, anaweza hata akatumia muda mwingi kwenye kioo kuliko kwenye maombi akijitengeneza, lakini bado mume wake asimtamani; kwa nini? Kwa sababu ndani yake hajaachia watu wa nyumba ya wazazi wake. Au watu wa nyumba ya baba yake wana nafasi kubwa moyoni kuliko mume wake.
Ni mabadiliko ambayo lazima uyatarajie, watu wengi sana huwa hawafikirii hayo, wanafikiri ni kitu rahisi. Unaweza sasa ukaelewa kwa nini watu wengine ikifika siku ile ya “send off”, yaani ya kum’send’ msichana ‘off’ asikae tena nyumbani kwa baba yake, hiyo siku ni ngumu sana kwa wazazi. Kwa sababu wanajua, wanaagana na msichana wao, mahusiano yao waliokuwa nayo toka mwanzoni, tangu alipozaliwa, alipokuwa tumboni mpaka wakati huo yanabadilishwa, yanajengwa mengine, sasa anakwenda kuwa mke wa mtu, hawawezi tena kuingilia maamuzi juu yake, amefunga agano mahali pengine.
Unakuta siku hiyo wazazi wengine wanalia, unakuta vijana wengine wanalia, wasichana wengine wanalia. Usije ukafikiri ni kitu rahisi. Ndani ya nafsi kuna vitu vinaachana, kati ya wazazi na wale watoto wanaoana.
JAMBO LA PILI: Unapoamua kuoa au kuolewa, fahamu ya kwamba hiyo ndoa inakuunganisha na kukuingiza katika familia nyingine.
Unafahamu watu wengi sana wakioa au kuolewa wanafikiria tu mahusiano ya wao wenyewe tu; na hii ni hatari sana. Kwa sababu unapooa unaingia kwenye undugu na familia nyingine kabisa tofauti, na sio mahusiano ya kwenu tu wawili. Ninyi ni kigezo tu cha kuunganisha hizo familia mbili, lakini mkiishaoana hizo familia zenu mbili ni ndugu kuanzia wakati huo.
Ndio maana unapofika unataka kuoa au kuolewa, sio suala la kumtazama kijana tu, au kumtazama msichana yeye mwenyewe tu; kwa mfano alivyosoma, lakini ni lazima pia utazame na hali ya familia yake ili ujue unajiingiza kwenye familia ya namna gani. Unapofika kwenye masuala ya namna hiyo kuna vitu vingi sana vya kuangalia.
Unaweza ukaingia kwenye familia ambayo ni wavivu, mimi ninakuambia jasho litakutoka ukioa msichana wa namna hiyo; au ukipata kijana toka kwenye familia ya namna hiyo. Itakuwa kazi sana kumshawishi mwenzako juu ya kujishughulisha na maisha. Maana inategemea; kwa kuwa unaweza kuoa msichana hata kusonga ugali hajui. Sisi kwenye nyumba ya baba yetu, hatuna msichana, tumezaliwa watoto wa kiume watupu, msichana wa kwanza kuingia kwenye familia yetu ni mke wangu.
Lakini mama yetu alikuwa na bidii ya kutufundisha kila kitu, alitufundisha kupika, alitufundisha kufuma, alitufundisha kusuka nywele. Kwa hiyo nilijifunza kwanza kusuka tatu kichwa. Lakini sikuanzia kujifunzia kusuka nywele kwenye kichwa cha mtu, bali nilijifunzia kwenye majani; wao wakikaa wanasuka hapo na sisi tuko hapo tunafundishwa jinsi ya kusuka kwenye majani.
Sasa wengine hawapati nafasi ya namna hiyo, na ni mbaya zaidi kwa wasichana. Mungu amenipa nafasi ya kuwa na watoto wakike watatu na wa kiume mmoja, itakuwa ni aibu kwetu kama wazazi, ikafika wakati wanaingia katika ndoa zao na hawajui kupika ni aibu; kwa hiyo lazima wajue kupika. Maana kwa kujua hilo anaonyesha anatoka familia ya namna gani, na imemlea kwa namna gani!
Unaweza ukafikiri unamlea mtoto wako vizuri, maana siku hizi kuna shida ya kuwa na wafanya kazi majumbani mwetu. Ukishakuwa na mfanyakazi nyumbani basi watoto wengine hawafanyi kitu, wakati mwingine wanakula chakula na wanaacha sahani hapo hapo mezani.
Kuna watoto wengine inakuwa mpaka yuko sekondari hawezi kufua nguo zake. Kwa kuwa nyumbani kama hakuna wa kumfulia basi kuna mashine za kufulia. Huko unakokwenda kuolewa inawezekana hata mashine ya kufulia hawajawahi kuiona! Unafika pale na unauliza mashine iko wapi, wanakuambia yakufanyia nini, ya kusagia mahindi? Maana ndio wanayoijua kuwa ndio mashine!
Hujui hata namna ya kushika kioo cha taa ya chemli wala namna ya kuiosha kule ndani lile vumbi likaondoka. Inawezekana mwingine umezaliwa kwenye nyumba yenye umeme, lakini utakapokuwa katika ndoa unaenda kwenye nyumba ambayo haina hata umeme, unafika kule na unashangaa kweli maana hujui hata namna kuwasha taa ya chemli! Kwa hiyo tunawaambia watoto wetu suala la kujifunza hivi vitu sio suala la kuchagua, hata kama kuna mtu pale nyumbani wa kuwasaidia, ni lazima wajue kufanya kazi!
Nilienda kwenye mkoa mmoja wakasema, sisi ukitaka kuoa kwenye nyumba ya mtu, ukitaka kujua huyo msichana amelelewa vizuri au vibaya wakasema usimtazame alivyovaa. Badala yake wanafika kwenye uwanja wa nyumba ya wazazi wake, na wanaangalia ile barabara inayokwenda nyumbani kwao, na wakiikuta chafu, basi wanajua huyu msichana ni mchafu, hawahangaiki tena kuja kuzungumza, wanajua hapa kama tunaamua kuoa tujue tunacho oa, huyu msichana ni mchafu!
Ukienda kuoa kwenye familia nyingine utakuta wanasumbuliwa na ugonjwa wa kurithi, na usipojua kitu cha kufanya unaweza ukapata shida sana. Lakini ninachotaka kukuambia ni kwamba, uamuzi wa kuoa au kuolewa unakuingiza kwenye familia nyingine kabisa, na inaunganisha hiyo familia yao na familia yako; kwa hiyo hayo sio maamuzi madogo. Kumbuka unapooa au kuolewa unawaingiza watu katika famila ambazo kama usipokuwa mwangalifu inaweza ikaleta shida sana, lakini pia inaweza ikaleta baraka!.
JAMBO LA TATU: Ukiamua kuoa au kuolewa, wakati mwingine imani yako inaweza ikabadilika.
Wasomaji wa biblia wanamfahamu mtu mmoja aliyeitwa mfalme Sulemani (unafahamu ni kwa nini aliandika kitabu cha Mhubiri, maana alipoandika kitabu cha Mhubiri akasema, mambo yote chini ya jua ni ubatili mtupu). Biblia inatuambia wazi kabisa ya kuwa Mungu alimpa hekima ya ajabu, na wasichana wakatoka sehemu mbali mbali duniani kwenda kufuatilia ile hekima, walipoikuta hawakutaka kuondoka na wakabaki pale kwake.
Kosa alilofanya Sulemani ni kwamba wale wasichana walikuwa wanakuja na miungu yao, na alikuwa anawakaribisha wale wasichana na miungu yao, anawapa na mahali pa kujengea vibanda vya miungu yao. Biblia inatuambia wazi kabisa, ilifika mahali wale wakina mama wakamgeuza moyo wake usiendelee kumpenda Bwana. Kitabu cha 1 Wafalme 11:4 kinasema hivi: “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”
Nimeona vijana wengi sana ambao wanakuwa moto sana kwenye wokovu kabla hawajaolewa au kuoa, wewe ngoja waingie kwenye ndoa na wafuatilie baada ya muda, utakuta wengine wamepoa mpaka wameganda kama barafu! Ukiwauliza ni nini kimewafanya wapoe kiroho kwa kiwango hicho, wanaweza wakashindwa kusema. Maana kuna watu wengine wanafikiri ni kuolewa tu na mtu yoyote kwa sababu tu anasema Bwana asifiwe, ibilisi Pia huwa anaweka na watu wa kwake huko ndani ya makundi ya watu waliookoka.
Na ukikaa na vijana utapata baadhi yao wanaosema, ukitaka kupata vijana waaminifu siku hizi nenda katikati ya waliokoka, kwa hiyo wanajifanya wameokoka. Akikufuatilia juu ya kuoana na ukimwambia mbona wewe hujaokoka, na ukamtaka kwanza aokoke ndipo mzungumze, utakuta baada ya siku chache kupita anajifanya ameokoka, lakini ni yakubabaisha tu ili akupate. Nimekutana na watu wa namna hiyo, msichana anaolewa akishafika ndani, ndio kijana anamwambia, na Yesu wako na wokovu wako nauvua hapa hapa, mimi nilikuwa nakutafuta wewe, nimekupata basi!
Nimeona! Sisemi kitu cha hadithi, ninasema kitu ambacho nimeona kwa macho. Ikiwa umefika katika hali hii basi, ni mpaka kifo kiwatenganishe, na alikwishawaambia wenzake kwamba Mungu amenifunulia; kwa hiyo hana ujasiri wa kurudi na kusema kweli nilikuwa nimekosea, yalikuwa ni mafuniko sio mafunuo! Akitaka kwenda kwenye maombi anaambiwa hakuna; akitaka kwenda kuhudumu anaambiwa hakuna; anataka kwenda “fellowship”, anaambiwa hakuna; kaa hapo ndani. Kwa hiyo inabaki kazi moja tu ya kuombea chakula na chai na kwenda kulala!
Na ni kwa sababu huyu mtu hakufikiri sawasawa, hakukaa akaona jinsi ambavyo hili jambo linaweza likambadilishia imani yake kabisa. Wewe nenda kwenye maandiko, utaona ya kuwa ndoa inaweza ikakubadilisha. Ndio maana kuna watu wengine wanaolewa, na wengine wanaoa na wanabadilisha dini, hii sio kitu cha mchezo, ni maamuzi magumu sana kuyafanya.
Unapobadilisha imani yako unabadilisha msingi wako kabisa wa maisha yako; kwa hiyo ni lazima uamue jambo ya kuoa au kuolewa kwa uangalifu sana.
Lakini pia inaweza ikawa ni mkristo kwa mkristo wanataka kuoana, lakini fahamu kuoa au kuolewa kunaweza kukakubadilisha dhehebu lako la kikristo, ndio maana lazima mkubaliane juu ya jambo hili kabla ya kuingia kwenye ndoa. Nilikuta vijana wamekubaliana kuoana, kijana mmoja mlutheri, kijana mwingine mpentekoste. Mambo yakawa magumu sana kwao, walipofika masuala ya kujadiliana, juu ya imani zao. Ilikuwa ngumu sana, mpaka wachungaji wao wakaingilia kati.
Walipokuja kuniona, nikawauliza mko tayari kabisa na mnataka kuoana? Wakasema, ndio. Wakati huo walipokuja kwangu walikuwa tayari wameshaenda nyumbani kwao, wameshazungumza na wazazi wao, na kote huko na wakati wote huo hawakufikiria hilo jambo. Sasa imefika mahali mchungaji wa kanisa hilo la pentekoste hakubali msichana wake aolewe kwa kijana wa kilutheri. Nikamuuliza maswali yule msichana akashindwa kujibu.
Unajua wapentekoste hawabatizi watoto, walutheri wanabatiza watoto. Mnapooana matokeo yake ni kwamba watoto watazaliwa. Ni lazima hicho kitu ufikiri kabla hajasema ndio kuolewa, au ndio kuoa. Sio umekwisha olewa ndipo unasema watoto wangu hawawezi kwenda huko, ulikuwa wapi toka mapema ili uliseme hili tatizo? Maana unaweza ukafikiri ni masuala marahisi, sio masuala marahisi.
Maana wengine wanalichukulia jambo hili kirahisi, wakati jambo lenyewe sio rahisi. Masuala ya kwenda kusali kanisa tofauti tofauti huku mmeoana sio mambo rahisi. Nimeona watu wakisema hakuna tatizo maana tutaoana, lakini kila mtu wetu atakuwa anakwenda kanisani kivyake; sawa, ninyi mnaweza mkaenda kivyenu, na watoto je? Labda kama hamna mpango wa kuzaa!
Maana niliona kwenye TV, mtu mmoja, dada mmoja huko ulaya amefuga mbwa akasema, tuliamua huku ndani tusizae watoto na badala yake tumefuga mbwa badala ya mtoto, wamempa na jina, wamempa na chumba wamempa na kitanda, anasahani yake, na bajeti yake, ana daktari, wameamua wasizae na badala yake, wamefuga mbwa! Labda kama unataka kuelekea njia hiyo! Lakini kama unaingia kwenye ndoa na unajua utakwenda kupata mtoto, suala la mahali mnapokwenda kusali ni muhimu sana kulijadili na kuliamua kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Usiende kupeleka vita kwenye ndoa yako ambayo haitakiwi kuwepo! Unajua kuna vita vingine tunavianzisha bila sababu, hata Yesu alijua, wakati saa yake ya kupigwa mawe ilipokuwa haijafika, alikuwa anawakwepa wale watu waliokuwa wamepanga kumpiga mawe. Sasa kama Yesu alikuwa anakwepa majaribu mengine kwa nini wewe unajitumbukiza? Saa ikifika ya jaribu kuja kwako utalishinda tu, kwa sababu umetengenezwa na Mungu uwe na uhakika wa ushindi, kwa sababu ukiwa ndani ya Kristo unashinda na zaidi ya kushinda.
Imeandikwa hivi katika kitabu cha Warumi 8:37; “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda”. Lakini majaribu ya kujitafutia, yanaweza yakayumbisha imani yako.
Maana watu wengi sana huwa hawajiulizi hili swali mapema lakini nimeona likiwapa shida. Wengine hata imefika saa ya kufunga ndoa, ndio kwanza wanaanza kujiuliza, ‘ndoa sasa tunakwenda kufungia wapi’, hilo sio swali la kujiuliza saa hiyo, utakuwa umechelewa! Wewe ulikuwa unajua kabisa mwenzako anasali mahali fulani, na wewe unasali mahali pengine, imefika saa mnataka kufunga ndoa mnaanza kujiuliza, tukafunge ndoa kwenye kanisa la nani, ikiishafika hapo mnaanza kushindana na kuvutana; na haifai mambo kuwa hivyo.
JAMBO LA NNE: Uamuzi wa kuoa au kuolewa ni muhimu uwe mwangalifu nao, kwa sababu utakufanya
uwajibike zaidi.
Kama hujawa mtu wa kuwajibika, basi, hujawa tayari kuwajibika, kwa hiyo usiingie kwenye ndoa! Kuoa au kuolewa kunakufanya uwajibike zaidi, maana yake ni kutafuta wajibu mkubwa zaidi.
1Timotheo 5:8 anasema, “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiye amini”, maana yake ni mbaya kuliko mtu ambaye hajaokoka. Afadhali mtu yule ambaye hajaokoka. Huyo ambaye ameokoka, lakini hatunzi watu wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, maana yake amemkana Yesu; ni mbaya kuliko hata mtu ambaye hajaokoka.
Hii inaonyesha ya kuwa unaweza ukaingia kwenye ndoa ukapoteza wokovu wako, ukakosa kwenda mbinguni, si kwa sababu umefanya dhambi ya uasherati, lakini kwa sababu umeshindwa kutunza watu wa nyumbani mwako, na kwa ajili hiyo unahesabika kuwa umeikana imani.
Ukiangali kwenye Tito.2:3-5 anasema, “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu, wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema, ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, na kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe, ili neno la Mungu lisitukanwe”.
Unaweza ukaona kabisa ya kwamba Timotheo, anazungumza habari za vijana wa kiume waliooa na wanafamilia, au umeoa na hujapata mtoto. Unao watu nyumbani mwako, inawezekana ni msichana umeolewa, huu mstari pia unakubana. Ukienda kwenye kitabu cha Tito, Tito anaandika moja kwa moja habari za wanawake wazee, ili wawasaidie wanawake vijana, maana yake wasichana ambao ndio wameolewa tu. Anasema, “Wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao”.
Usingetegemea msichana aambiwe awapende watoto wao, hutaona mwanaume anaambiwa awapende watoto, bali anaambiwa awalee watoto. Mwanamke anaambiwa awapende watoto, ni kitu ninashangaa kila siku; maana nisingetegemea mama aliyepata uchungu wa kuzaa aambiwe ampende mtoto. Watu waliookoka wengi hasa wanapoingia kwenye ndoa, wanaingia kienyeji kienyeji tu, hawajali ya kwamba kuna kuwajibika.
Huwa ninawaambia vijana siku zote, hata kama mlikuwa mmezoea kutokula nyumbani mwako, (maana kijana akiwa bado hajaoa, anaweza akakaa wiki au wiki mbili, jiko lake halijawahi kupika kitu); kijana akiwa bado hajaoa, hakimsumbui ana hela au hana hela, ataishi. Chakula kikiisha anaenda kutembelea ndugu na jamaa, kama hawataki kumpa chakula, atakaa hapo mpaka amekula na ndipo aondoke. Akikosa kabisa atajitia moyo kwa Bwana kwamba amefunga, na kumbe ameshinda njaa!
Wakati mwingine mambo yakimzidia, na hana sabuni ya kufulia nguo anasema hajali, kwa hiyo anaendelea, hana shida, anabadilisha nguo sio kwa sababu amefua, lakini anabadilisha ili angalao jasho liweze kupungua hasa mnuko wake, kwa hiyo anaitundika mahali ipigwe upepo usiku; na baada ya siku mbili anavaa hiyo hiyo tena!
Huwa ninawaambia vijana siku zote kama hauko tayari kuwajibika, usioe. Kwa sababu kama umeoa, haijalishi ya kwamba unafunga au hufungi, chakula lazima kiwemo nyumbani mwenu. h haleluya! Na ukishaoa tu, maana yake umeitangazia dunia nzima ya kuwa umeamua kuwajibika, na unaweza ukatunza mke. Mambo ya kwenda kuomba -omba msaada tena inakuwa ni kitu ambacho si wakati wake sasa. Maana unaposema, mimi nimeamua kuoa, maana yake umekubali kuwajibika na hii ni pamoja na kumlisha na kumtunza mke wako.
Ndio maana ukienda kwenye makabila mengine wanakuambia, ‘kijana unataka kuoa umejenga nyumba?’ Nimeona makabila mengine wanauliza, ‘kijana wewe utaoaje wakati hata nyumba huna?’ Ndio maana vijana wanazuiwa kuoa wakiwa shule, kwa nini, kwa sababu katika ndoa watahitaji kuwajibika. Sio kwa sababu wakiwa shule hawawezi kuoa, ila ni kwa sababu wanajua suala la kuoa sio kitu cha mchezo, linahitaji mahali ambapo unahitaji kuwajibika. Ndani yako lazima uwe umekubali kuubeba wajibu uliomo katika ndoa!
Na kama ni msichana unataka kuolewa ukubali kuwajibika basi la sivyo usikubali kuolewa kama hujawa tayari kuwajibika. Tito anawaambia wazi kabisa, ya kuwa wafanye kazi nyumbani mwao wenyewe. Lakini sasa unataka hata kama umeolewa, uishi maisha kama msichana, na hiyo ni hatari sana. Ukiingia kule ndani ya ndoa kuna mabadiliko. Wakati ule ulikuwa unaosha vyombo vichache maana ni vya kwako peke yako, sasa na mume wako yuko, na marafiki zake wamekuja, vyombo vya kuosha vitaongezeka, na kuwajibika kwako kunaongezeka.
Ilikuwa inakusumbua kupika, unapika mara moja kutwa, na siku hizi wataalamu wametuletea kitu kinaitwa ‘hot pot’, kwa hiyo hii mambo ya kupasha pasha moto chakula siku hizi wakati mwingine hayahitajiki. Mtu ameweka chakula chake anakifunika vizuri, anakuja jioni anakuta bado cha moto. Lakini ninakuambia labda umeingia umeolewa na mtu ambaye ni mtumishi, ana wageni nyumbani kwake kama kituo cha polisi, kila baada ya dakika mbili amekuja na wageni wengine.
Labda mume wako ni mkarimu sana, kila mgeni akija anakuambia, “fulani chai vipi?” Huko jikoni ‘unauma vidole’ maana umeshaingia jikoni kuanzia asubuhi; labda saa hiyo ni saa tano, na umeshaingia jikoni kupika mara nyingi, maana wageni wanapishana kila wakati. Kila saa ‘chai, chai’, unatamani uondoke ili usiendelee kupika, lakini umebanwa, ndio kuolewa kwenyewe huko. Ukiamua kuolewa kuwajibika kwako jikoni kutoangezeka zaidi.
Huwezi ukaamua tu saa yoyote ukasema, mimi nataka kwenda kutengeneza nywele, huo muda wa uhuru wa jinsi hiyo umekwisha, ukitaka kwenda kutengeneza nywele lazima uage, huwezi ukaondoka tu saa yoyote unayotaka, kila kitu kinabadilika. Kuna masuala ambayo utahitaji kuwajibika nayo pale nyumbani, huwezi kukwepa! Na kuna mambo mengine hakuna mtu mwingine ambaye atafanya kwa niaba yako; kama usipotaka kuyafanya wewe.
Ndio maana watu wanafika mahali, msichana anaolewa lakini wiki ya kwanza tu anataka msichana wa kazi wakati, hana hata mtoto mdogo. Unataka msichana wa kazi wa nini, huo ni uvuvi tu. Lazima uwe mwangalifu, wewe umeolewa tu, unataka msichana wa kazi, wa nini? Unaweza ukajitetea na kusema ni kukusaidia kazi, kazi zipi? Unaweza ukajitetea na kusema, aa! Unajua ninachelewa sana kutoka kazini, angalao nikute mtu wa kupika. Mimi ninakumbia unaanza vibaya. Kama ndiyo kwanza umeolewa tu, na unataka wakumpikia chakula mume wako awe ni msichana wa kazi, basi unaanza vibaya.
Wakati huo ndio saa ya kumtayarishia mume wako mapishi ambayo hajawahi kuona kwenye nyumba ya baba na mama yake! Akikaa mwenyewe huku anakula awe anasema, ‘ahsante Yesu kwa kunipa msichana wa namna hii!’ Kwa sababu hajawahi kuona chakula kizuri cha namna hiyo ulichompikia hata hoteli hajawahi kukipata!
Lakini unaanza tu maisha ya ndoa na kumbandikia mume wako watu wa kumhudumia, mimi ninakuambia unaanza vibaya, huko unakoelekea na ndoa yako sio kuzuri. Uamuzi wa kuoa au kuolewa usiucheezee, kaa chini, fikiri kwanza na kuomba kabla hujaamua.
JAMBO LA TANO: Uamuzi wa kuoa au kuolewa, unaweza ukabadilisha utumishi wako na wito wako kabisa
Ngoja nikutolee mfano wa kibiblia. Unamkumbuka mtu mmoja aliyeitwa Samson, alimwoa dada mmoja aliyeitwa Delila, utumishi wake ulinyongewa huko kwenye maisha yao ya ndoa. Ukisoma kile kitabu cha Waamuzi.16:21 kinasema hivi, “Wafilisti wakamkamata wakamng’oa macho, wakateremka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba naye alikuwa akisaga ngano katika gereza”.
Unajua huyu alikuwa ni mtumishi wa Mungu mzuri kabisa. Lakini hakujua ya kwamba yule mwanamke aliyempenda na akamwoa aishi naye alikuwa ni ‘ajenti’. Hakujua ya kuwa yule dada alikuwa ni ‘ajenti’ wa adui. Yule dada alikuwa ni ‘ajenti’; kabisa akambembeleza mume wake amweleze siri ya nguvu zake, lakini Samsoni mwenyewe alikuwa anaficha kusema siri ya nguvu zake iko wapi. Lakini yule dada alikuwa na ujuzi wa kubembeleza. Akambembeleza yule baba kiasi ambacho akashindwa kuficha siri yake, na akaisema.
Unajua inapofika kwenye masuala ya ndoa inatakiwa muweze kusaidiana, mtu asitumie udhaifu wako kukuangusha, mtu asitumie udhaifu wako kukuzamisha, mtu asitumie makosa yako kukupeleka jehanamu, inatakiwa ukimpata mwenzako ukiwa na udhaifu akusaidie, ukiwa kwenye dhambi akuombee utoke, unaelekea jehanamu akusaidie kwenda mbinguni, ndivyo inavyotakiwa iwe kwenye ndoa.
Lakini ninakuambia ukimpata mtu, na wewe una maisha yanayoelekea jehanamu, anakuambia nenda salama, hii ni hatari. Yule dada alikuwa anamfuatilia Samsoni kumnyang’anya kitu kilichokuwa ndani yake cha utumishi alichokuwa amepewa na Mungu, na Samsoni hakujua. Alipofika mahali pa kuisema siri yake alifikiri mke wake ni mwenzake ambaye anaweza akampa siri yake vizuri bila shida.
Ndio maana kwenye ndoa ambazo watu hawaaminiani vizuri, siri zao hawaambiani. Na ikishafika kwenye ndoa, mnasiri mlizozifichana iko shida, maana yake kuna eneo ambalo usingetaka liingiliwe, unafunga na ufunguo, kasha unatembea na ufunguo mfukoni. Ni eneo umeficha, kwenye ndoa mnatakiwa mfahamiane kila siku, na udhaifu wako, na shida ilioko, na matatizo yaliyoko, kila kitu kiwepo peupe, ili mwenzako atafute namna ya kukusaidia.
Samsoni aliona kitu cha tofauti, lakini alikuwa mke wake, maadui wakaja wakamshika, mke wake anatazama na kushangilia. Badala ya Samsoni kumtumikia Mungu, akaenda akawa anasaga ngano gerezani. Biblia inasema wakamtoboa macho. Kwa jinsi ya rohoni ningekuambia, wanaondoa macho yako ya rohoni, maono ya Kimungu yanapotea, mtazamo wa Kimungu unapotea, mipango ya Kimungu inapotea.
Ndio maana unakuta mtu ameolewa ameokoka, au ameoa huku ameokoka, akifika ndani ya ndoa maono ya Kimungu yanapotea, na utumishi wake unazama. Anabaki kusema ‘Bwana asifiwe’, kama bado anaweza akaendelea kusema ‘Bwana asifiwe’, lakini ndani ya moyo amenyonywa kiroho na hakuna kitu.
Sasa labda na ninyi ni mashahidi, wewe angalia vijana ambao wameoa na kuolewa, angalia kama bado wanao moto ule ule wa utumishi, ambao walikuwa nao kabla hawajaingia kwenye ndoa. Wengine wanabaki kumsingizia Mungu ya kuwa, ameesbadilishia huduma, wakati sio Mungu, kumbe ni mume wake amembadilishia huduma, au ni mke wake tu amembadilishia huduma! Maana hakuhesabu gharama ya ndoa kwenye wito wake.
Kwa mfano; Mke wako anakutaka nyumbani, huduma inakutaka kila siku uwepo barabarani, usije ukafikiri ni kitu kirahisi hicho. Utafika mahali lazima uamue, unataka kumpendezesha mke wako au unataka kumpendezesha Mungu.Haya si mambo ambayo ni rahisi kuyaweka vizuri na kuyaanisha bila msaada wa Mungu. Na kama alikuwa anajua anaolewa wapi, kusumbuliwa suala la kusafiri kwako kwenye huduma lisingekuwepo, angekua anakutia moyo na kukuombea, na kukusindikiza siku nyingine. Lakini inapofika anaanza kupata shida, maana yake kuoana kwenu kuna kasoro mahali, na kumekuwa mzigo.
JAMBO LA SITA: Uamuzi wa kuoa au kuolewa unaweza wakati mwingine kukuletea marafiki au maadui.
Sasa nakufikirisha hivi vitu vikusaidie, inawezekana kabisa hujafikia umri wa kuoa au kuolewa, lakini ninakuambia weka maombi yako ya akiba, (sijui kwa upande wako, lakini mara nyingine huwa nawaombea watoto wangu maombi ya akiba, kwa ajili ya ndoa zao kama Yesu atakuwa hajarudi, kwa sababu najua maana yake ni nini).
Ni vizuri upate maombi ya namna hii mara kwa mara ujiombee mwenyewe, ukipata watu wa kukuombea shukuru Mungu, lakini hata kama hujapata watu wa kukuombea, ninakuambia kazana kujiwekea maombi ya akiba. Hiyo ni njia panda. Mahali pa kuoa au kuolewa ni njia panda. Ukichagua njia ambayo haiko sawasawa, maisha yako yatakuwa magumu sana.
Sasa ukiangalia kwenye kitabu cha Hesabu 12:1-2 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao” inatuonesha wazi kabisa ya kwamba, harusi ya Musa ilileta ugomvi katikati yake na ndugu zake, hasa dada yake na Haruni. Kilichowasumbua ni kwamba alikwenda kuoa mwanamke Mkushi; au amekwenda kuoa mahali ambako hawakutarajia, kwa hiyo wakakasirika. Halafu naamini Musa aliwaambia Mungu amesema naye juu ya kuoa mke huyu, wale watu wakasema, “Mungu anasema na Musa tu peke yake, haiwezekani” ugomvi ukaingia.
Unajua ugomvi uliingia kiasi ambacho Mungu akasikia yale maneno na hayakumfurahisha, akawaita kwenye hema. Ikabidi ajieleze wazi uhusiano wake na Musa.
Kitabu cha Hesabu 12:6-8 kinasema; “Kisha akawaambia, Sikilizeni basi maneno basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?” Alivyomaliza kusema namna hiyo dada yake Musa akapata ukoma!
Ugomvi umetokea wapi? Musa alipooa! Kwa kuwa ameoa msichana ambaye dada yake hakumtaka. Mungu alimtaka, lakini dada yake hakumtaka. Dada mtu akaanza kumsema kaka yake, Mungu akampa adhabu! Dada mtu alipopewa adhabu ile na kaka mtu akapata shida, Israeli nzima ikapata shida, hawakusafiri walisimama wote, hawakuendelea na safari. Ugomvi ulitokea wapi? Ulitokea mtu mmoja alipooa!
Nimeona ndoa zingine kijana anaoa lakini uhusiano wake na baba yake na mama yake unakatika wakati huo huo. Vijana wengine wanakuwa hawako waangalifu hapo, na ndio maana mambo yakiwa magumu, na wazazi wanawabishia juu ya kuoa au kuolewa kwao hawataki kwenda kuzungumza na wazazi wao; wanapiga “short cut”, wazazi wao wanakuja kuambiwa tu saa na tarehe ya harusi!
Biblia inasema, “waheshimu baba na mama yako, hii ni amri ya kwanza yenye ahadi ili upewe siku nyingi katika nchi upewayo na Mungu wako” - Waefeso 6:1. Na kwa sababu hiyo vijana wengi sana wakiishakorofishana wazazi wao hawaendelei katika ndoa muda mrefu wakiwa na amani.
Sasa sisemi kwamba wamkubali tu huyo msichana au huyo kijana, ni zaidi ya hapo unajua. Suala ninalozungumzia hapa ni la wao kukupa kibali, na wakafurahi. Unaweza ukasema, hawaelewi kitu au hawajaokoka, kwa hiyo hawahitaji kuelezwa kitu. Hapana!
Ndio maana unahitaji kuomba. Kwa sababu unajua suala la kutaka kuleta msichana au kijana ndani, sio la kwako peke yako, linawahusu wazazi wako na ndugu zako kwa sababu unawaingiza kwenye familia nyingine. Hata kama unataka kuoa au unataka kuolewa, ni mambo ya kifamilia maana ni koo mbili zinakutanishwa na kuunganishwa.
Wakati mwingine unaunganisha kabila mbili au unaunganisha kabila tatu, (wengine hawaelewi kitu ninachosema, kwa mfano; “Mimi ni mnyakyusa, mke wangu ni msukuma, watoto wangu ni kabila gani”? Wanakabila mbili, ni mchanganyiko wa wanyakyusa na wasukuma, maana ningetaka kujipendelea ningesema ni wanyakyusa.
Lakini ndani wanaunyakyusa na wanausukuma halafu waolewe na mtu wa kabila lingine ambalo sio mnyakyusa wala sio msukuma, ni makabila mangapi yanaungana hapo, matatu! Sasa fikiria na anayeoa kwangu na yeye awe ametoka kwenye mchanganyiko wa namna hiyo.
Unaunganisha hapo makabila matatu, manne, matano, sasa wewe unataka wazazi wako wasiifuatilie ndoa hiyo kwa karibu. Kwa nini? Ukipata shida utarudi kwa wazazi wako, sasa kwa nini wakati wa maamuzi wasikusaidie!
Na mimi ninakuambia iko njia ya kutokea, ikiwa utapata tatizo la namna hii; wewe kukaa kwenye maombi kwa namna ambavyo, kama ni Mungu kweli aliyekupa huyo msichana au aliyekupa huyo kijana, basi ataweka kibali hicho hicho ndani ya wazazi wako, ili na wao wamkubali.
Saa nyingine unaweza ukapata marafiki wengine wazuri, lakini wakati mwingine marafiki wengine wanakuwa ni wabaya. Maana ukishaolewa marafiki wa mume wako ni marafiki zako, ukishaoa marafiki wa msichana ni marafiki zako. Vijana siku hizi wanaotaka kuoa au kuolewa wakitaka kujua ukoje, hawakuangalii wewe wanaangalia marafiki zako. Marafiki ulionao ndio wanaoonyesha picha uliyonayo ndani yako.
Rafiki wa kweli hafuati pesa ulizonazo, anafuata tabia uliyo nayo, wale marafiki wanaokufuata kwa sababu unacho kitu cha kuwapa hao sio marafiki, wanakufuata kwa sababu unachokitu, siku ukiishiwa huwaoni. Lakini wale marafiki unakuwa nao wakati wa shida na wakati wa raha, ni marafiki ambao malengo yenu na tabia zenu, kufikiri kwenu kusema kwenu zinafanana. Hao ndio marafiki ambao wanakuwa marafiki zako wa kweli; siku ukiwa na shida ni marafiki zako, unahela ni marafiki zako, umefilisika ni marafiki zako, hao ndio marafiki zako!
Sasa kama mtu anataka kukuangalia ulivyo, anaangalia marafiki zako. Sasa, akiangalia marafiki zako, hata kama unasema, ‘Bwana asifiwe’, hata kama unapiga pambio mpaka jasho la damu linatoka, lakini wanaangalia marafiki zako ulionao, na wakati mwingine ni wabaya kuliko wale wa kule duniani, wanajua na huyu msichana au huyu mvulana kuna mahali ‘ana short’.
Kwa wengine inakuwa vigumu kuliona kwa namna hii, lakini ni lazima ufahamu ukiwa kama kijana, lazima uwe mwangalifu juu ya marafiki ulionao. Vijana wengine wanabaki kushangaa kwa nini wasichana wanahangaika wanasema hatuoni vijana wa kuwaoa, wakati vijana wapo, lakini nani ataolewa na vijana ambao wameokoka lakini hawana msimamo? Nani anataka kijana wa namna hiyo ambaye anashinda vijiweni sawasawa na hao vijana wengine wa duniani?
Mwanaume akitaka kuoa lazima ajifunze kuwajibika. Hawezi akawa na marafiki ambao hawawajibiki kimaisha na akataka aone na aendelee na urafiki nao. Akiwa karibu na hao marafiki, itakuwa ni vigumu kuwa na ndoa yenye amani. Angalia tu marafiki alionao, unashangaa kwamba anaendelea kusema bado ameokoka.
Unashangaa wale marafiki alionao, hawafananii, hawawezi hata kumtia moyo kuomba, hawawezi kumtia moyo kusoma neno, vitu wanavyozungumza ni vitu vya ajabu.
Unajua, hata wakati mmoja hawana maneno ya kutiana moyo ya kuwa na maendeleo binafsi, lakini ndio anaoshinda nao toka asubuhi mpaka jioni, halafu anataka kuoa msichana ambaye ameokoka, anayeshinda kwa Mungu, anayekaa kwenye maombi, anayetaka kuona cha Mungu kinasimama katika maisha yake, ndiye anataka kwenda kwake ili amuoe;- hii siyo sawa! Ndoa yao itakuwa na matatizo tu kwa muda mrefu.
Maana usije ukapata shida ukiingia kwenye ndoa na kijana wa namna hiyo. Wewe uliona kabisa marafiki zake walivyo, unaolewa na ndipo unaposema, ‘mimi sitaki hao marafiki zako’! Imeanza wapi? Atakuambia vizuri kabisa “ulinikuta nao”, kwa nini hukusema mapema kabla hatujaoana ya kuwa huwataki?
Msichana anaolewa na ndipo kijana anamwambia hao marafiki zako nisiwaone hapa, lakini alikuwa anawakuta chumbani kwako wakati alipokuwa anakuja kukutembelea na hakusema kitu, na wakati mambo yakiwa magumu katikati yenu alikuwa anawatumia wao kukubembeleza ukubali kuolewa naye, sasa umekwishaolewa hawataki. Anaanza kuwasema ya kuwa tabia zao sio nzuri. Hili jambo si zuri; alitakiwa aseme mapema juu ya kutoridhika kwake na rafiki zake.
Unapotaka kuoa au kuolewa, usifikirie tu picha ya yule mtu wakumuoa au kuolewa naye, ni vizuri kuangalia na aina ya marafiki zake wa karibu – je unaweza kuchukuliana nao?.
JAMBO LA SABA: Je! Uko tayari kuoa au kuolewa?
Ni swali muhimu, uko tayari, maana yake umefika mahali hali yako ya ndani na nje, inakuruhusu kuoa au kuolewa? Uko tayari kuoa au kuolewa? Umefika mahali pa namna hiyo?. Wengine wanasema huyu ni mtoto, lakini unajua pamoja na kwamba ni mtoto, ni vizuri kujua kama uko tayari kiumri. Lakini ninapozungumzia hapa juu ya utayari wa kuoa au kuolewa, sizungumzii tu habari za miaka, bali ninazungumzia habari za hali yako ya ndani.
Nimeona kuna mtu mwingine ana miaka arobaini, lakini kwa kweli hayuko tayari kukaa na mwanamke, ndani yake, mawazo yake na kufikiri kwake, hayuko tayari kukaa na mwanamke, hawajibiki hata yeye mwenyewe juu yake mwenyewe. Wengine hata wana miaka hamsini, lakini ana hali kama hii. Nimeona akinadada hata wana miaka arobaini na tano, hayuko tayari kuolewa, maana akiolewa ni shida tu.
Nilienda mahali fulani, nikakuta dada ana umri mkubwa tu, lakini wakati wa maombi hakusema kama anataka tuombe ili aolewe. Nikaona ngoja nimuulize labda anaona aibu kusema hitaji hili kwa sababu umri umesogea, nikamwambia “hutaki tuombe uolewe”? Akasema, “hapana, sitaki kuolewa” (Na alikuwa ana umri wa miaka kama arobaini na zaidi). Nikamuuliza, “kwa nini”. Akasema, “kwa sababu sitaki kuomba ruhusa kwa mwanaume ninapotaka kutumika”. Nikamuuliza unafanya kazi, akasema, “ndio”. Nikamwambia, “unapokwenda kumtumikia Mungu huwa unafanyaje, unaomba ruhusa au unatoroka huko kazini?” Akasema, “ninaomba ruhusa”. Nikwamwambia, “kwa nini unaona ni rahisi kuomba ruhusa kwa mwajiri wako na unaona taabu kuomba ruhusa kwa mume wako?” Alishindwa kujibu hilo swali.
Nikamwambia tatizo lako ni kubwa kuliko unavyo fikiri.
Unaweza ukaona kabisa ya kwamba, huyu mtu hayuko tayari kuolewa, wala msijaribu kumlazimisha aoelewe pamoja na kwamba umri wake ni mkubwa. Usijaribu kumsukuma kwenye maamuzi ya kuolewa maana hayuko tayari kuolewa, akiingia kwenye ndoa atakwenda kuleta shida tu!
Ndio maana ninakuuliza swali, je uko tayari kuoa au kuolewa? Lina vipengele vingi vya kulitazama, na linabadilisha vitu vingi sana.
Mwingine unakuta ni msichana, wazazi wake ndio wanamtegemea karibu katika kila kitu. Mimi ninakuambia kabla hujafikiria kuoa au kuolewa, fikiria hilo swali. Kwa sababu ukiishaolewa tu biblia inakuambia wasahau watu wa nyumbani mwa wazazi wako - Zaburi 45:10 “Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako”. Sasa haimaanishi usiwasaidie, ila maana yake ni kwamba huwezi ukawasaidia tena “moja kwa moja” kama ulivyokuwa unawasaidia zamani. Ni vitu lazima ujadiliane na mume wako juu ya kuwasaidia wazazi wenu wa pande zote mbili maana mna mipango yenu sasa.
Na inawezekana labda umeoa au umeolewa kwa kijana ambaye hana mzigo na wazazi wake kabisa, kila mtu anaishi kivyake vyake kama simba porini, suala la kusaidia wazazi hana ndani ya moyo wake. Wewe umekuwa na huo mzigo, wazazi wako wamekulea, umefika mahali umeanza kazi, sasa na wewe unawatunza hatua kwa hatua, siku unaolewa yule baba anasema basi usiwatunze tena, fikiri hilo.
Litakuwa linakuumiza kila siku jinsi wazazi wako wanavyopata shida. Utafika mahali utakuwa unachukua vitu kisiri siri unapeleka kwa wazazi, na hiyo ina shida yake pia. Kwa hiyo kabla hujakubali kusema mimi nataka kuolewa, fikiri kwanza na kuomba, maana ndoa inakwenda kukubadilishia mambo yako mengi.
JAMBO LA NANE: Je! Uko tayari kuolewa na nani?
Wengine hawafikirii namna hiyo, ukiwauliza uko tayari kuolewa na nani, anasema na mtu aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu kwa jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa alivyo kitabia. Maana watu wengi sana wanasema wameokoka lakini hawajaokoka, wengine wanasema ‘bwana asifiwe’ lakini ni bwana mwingine sio Bwana Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa kufikiri, unataka kuolewa na nani.
Labda hujawahi kufikiria kitu cha namna hiyo, nataka nikufikirishe vitu vya kawaida kabisa. Wengine wanasema mimi nataka kuolewa na mtumishi, hesabu gharama kwanza! Wengine wanaona tunavyoshirikiana na mke wangu katika huduma wanamtazama wanasema, wanataka kuolewa na mtumishi; kaamuulize mke wangu, tulipokutana hata wito haukuweko, na tulikutana wote hatujaokoka. Tulikuja kuokoka baada ya kuoana!
Mungu ametuteremshia utumishi tuko kwenye ndoa tayari, kwa hiyo usitamani ndoa ya kwetu, tamani ya kwako ambayo Mungu amekupangia. Mke wangu hakunipendea utumishi, sikuwa na tone la utumishi, wala hata ya kufanania ya kwamba nitaokoka, na yeye alikuwa hajaokoka pia wakati huo. Lakini kwa saa na kwa makusudi na kwa utaratibu wa Mungu, tumekuwa jinsi tulivyo. Akatuteremshia utumishi wakati tumekwishaokoka na tumekwishaoana!
Usijaribu kufananisha ndoa yako na ndoa ya mtu mwingine, hujui iliko toka, tamani ya kwako. Sasa unasema wewe unataka mtumishi, lakini watumishi wako wengi sana, kwa hiyo unataka mtumishi wa namna gani? Lazima ufikiri juu ya hili pia. Unasema mimi ninataka mhubiri, hata nabii ni mhubiri, mwinjilisti ni muhubiri, mwalimu anaweza akahubiri. Kitabia hawafanani, haleluya! Nataka nikufikirishe ikusaidie, maana nataka nikujengee msingi mzuri wa maisha ambao ukikanyaga vizuri shetani alie tu, maana hatawezi kukuvuruga.
Maana watu wengi wanapata shida sana wanapotaka kuoa au kuolewa, utakuta wanasema, mimi ninataka kuoa au kuolewa na mtumishi, hayo ni maombi ya mtu ambaye hajaenda shule ya Roho Mtakatitu, bado yuko chekechea, unajua lazima uwe ‘very specific’. Mungu anataka useme naye kile kitu unachokisikia ndani yako. Anajua kabisa kitu ambacho ni kizuri kwa ajili yako; lakini Mungu hataki kukulazimishia tu, anataka ushirikiane naye, ili akikupa kitu ukipokee kwa furaha.
Kwa hiyo kama unataka mtumishi, ni muhimu useme unataka mtumishi wa aina gani. Kwa mfano ukisema nataka mwinjilisti, hesabu gharama, lazima uwe na neema ya kukaa na mwinjilisti. Si unajua mwinjilisti hakai nyumbani, anazunguka, akikosa watu wa kuwachapa injili huko nje, anakuja kuchapa injili nyumbani hata kama mmeokoka wote! Na ujue hawezi kumaliza ibada ya jioni mpaka awepo mtu wa kutubu, hajatubu ataendelea kufanya maombi. Kama hauko tayari kuchukuliana na mtu wa namna hiyo usiamue kuoa au kuolewa naye.
Lazima useme; au kama unataka kuolewa na nabii jipange, kwa sababu hajui kuongea na watu, muda wake mwingi yuko kimya, manabii mara nyingi wanafungwa midomo sio wasemaji ni mtu mkimya. Mara nyingi amejifungia kuomba peke yake na Mungu.
Hata saa nyingine unatamani uombe pamoja naye, lakini Mungu anataka yeye peke yake. Wewe nenda kwenye biblia utaona maisha yake yalivyo kila kitu kinachomzunguka,kila kitu anachovaa, kila kitu anachokutana nacho, Mungu anaweza akakigeuza ujumbe.
Kwa hiyo usije ukashangaa kesho akakutazama na akaishia kupata mahubiri toka kwako, halafu mkirudi nyumbani mnaanza kugombana, na unamuuliza sasa wewe ulikuwa unanihubirije? Kwani wewe hukujua ya kwamba ni nabii na anaweza kupata ujumbe unaosema: “kama vile mke wako alivyovaa, ndivyo na kanisa langu lilivyo asema, Bwana”!
Wewe usifanye mchezo! Sasa nyingine mnaishiwa chakula na anaona jinsi mnavyohangaika, basi utakuta amekwishapata ujumbe kama huu, “kama vile mke wako alivyokuwa anahangaika kutafuta chakula kwa ajili ya watoto, ndivyo na mimi ninavyotafuta chakula kwa ajili ya watoto wangu, asema Bwana”!
Saa nyingine unavaa nguo zinapasuliwa, mpaka viungo vya ndani vinaonekana, ujumbe unatoka saa hiyo mara moja, anasema, “Kama vile mke wako alivyovaa nguo iliyopasuliwa na watu wanaona ndani, ndivyo na kanisa langu lilivyo vazi lake limepasuliwa na shetani anaona ndani”!
Lazima uwe tayari kuwa ujumbe, kama unataka kuolewa na nabii. Uwe tayari kuwa ujumbe, hujawa tayari usiombe uolewe na nabii! Unataka kuolewa na mchungaji uwe na moyo mkubwa wa kupokea wageni. Mwingine anasema mimi ninataka kuolewa na mtumishi lakini ndani yake anawaza mtu anayezunguka na kuhubiri, kumbe Mungu ameweka ndani yake mtumishi, lakini ni mfanya biashara.
Mfanya biashara mwingine anapakwa mafuta kufanya biashara, ndio sehemu yake kumtumikia Mungu, mwingine ni fundi cherehani, mwingine ni dereva, wanapakwa mafuta sehemu zao hizo za utumishi, usije ukafikiri hao wanaoafanya kazi nyingine sio watumishi wa Mungu. Mungu anawapaka mafuta kwa ajili ya hizo kazi, ili walitumikie kusudi lake.
Kwa hiyo unapokwenda katika maombi unasema tu mimi ninaomba mtumishi, Mungu atakuletea mtumishi yoyote, wako wengi, wengine wanafagia barabara, ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha kule kwenye vyoo vya kulipia ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha nyumba za watu, nao ni watumishi wa Mungu,oh haleluya!
Mungu akikuletea mtumishi yeyote unaishia kusema, mimi sikuomba huyu niliomba mtumishi. Mungu atakuambia huyu ni mtumishi wangu, usimnenee kitu cha namna hiyo.
Kama msichana ni mfupi usitamani kijana mrefu, au kijana ni mrefu unatamani msichana mfupi. Kwa kweli, sio kwamba Mungu hawezi kukupa, lakini wewe fikiri tu mwenyewe, haleluya! Maana mwingine anakuwa mfupi kiasi ambacho anafanana kama vile ni mtoto kwako, wenzako wanakuuliza tangu lini umepata mtoto na akakua na akawa mkubwa namna hii, unasema “ninyi msiseme hivyo, ni mume wangu huyu”. Ni uamuzi wako. Sasa, si lazima mfanane urefu, lakini msipishane sana; kwa kweli ni kwa faida yenu wenyewe, haleluya!
Kama msichana hupendi mwanaume mwenye ndevu, omba vizuri. Maana unaweza ukapata mtumishi wa Mungu, lakini ana ndevu na wewe huzitaki. Ikifika siku umeingia tu kwenye ndoa kitu cha kwanza unamtafutia wembe ili anyoe ndevu zake hii ni kumwonea! Ulimpenda akiwa na ndevu, kumbe wewe ulikuwa unamtegea tu ili baada ya harusi tu umpe wembe! Wako wasichana wanaopenda wanaume wenye ndevu, waachie hao!
Huyu Bwana Mungu wetu ni mzuri sana, unajua, saa nyingine huwa ninawaza jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na nabaki ninashangaa sana. Maana kuna wanaume wengine hata ndevu hawana, hata wakilazimishia kunyoa kidevu kitupu haziji. Sasa mtu mwingine anajisikia vibaya, akifikiri ya kuwa mtu anaonekana ya kwamba yeye ni mwanaume kwa sababu tu ana ndevu, si kweli. Kuna wanaume wengine wametengenezwa namna hiyo ‘special’ kwa ajili ya wasichana wasiotaka wanaume wenye ndevu, haleluya!
Maana mwingine anaweza akaachia ndevu zikafunika mpaka karibu na kwenye pua. Sasa kama ni mtu mweusi sana ‘ni hatari sana’, giza likiingia tu ndani ya nyumba wewe unamwambia ‘cheka’, akicheka yale meno yake yanaweza yakamulika kidogo, na utajua yuko wapi! Hivi vitu ukishaingia kwenye ndoa ni vitu vikubwa sana, kuliko watu wanapoviangalia kabla hawajaoana.
Wewe unakuta kijana anaoa msichana ana rangi nyeusi nzuri tu, akifika ndani unamletea madawa ajikoboe, wewe ulikuwa unamwoa wa nini? Hiyo sasa ni sawa na kumwambia Mungu kwa kweli nimechukua tu huyu, lakini sio niliyekuwa namtaka!
Niliyekuwa namtaka ni mweupe, sasa maandamu umenipa huyu wacha nimkoboe mpaka afike rangi ninayotaka, haviendi namna hiyo bwana! Mungu alipokuwa anamuumba huyo msichana namna hiyo aliona, alimtazama alivyo na weusi wake huo akaona kila kitu chema, akajipa sifa, akajipa maksi asilimia mia moja, amefanya kitu chema!
Sasa akitaka kupaka rangi hiyo ‘nyumba yake’ na kuinakshi ni kitu kingine. Unajua kuna nyumba nyingine hazipendezi mpaka uzipake rangi fulani, haleluya! Mwili ni nyumba, kuna wengine hawawezi kupendeza mpaka wamepaka rangi fulani kwenye miili yao. Sasa utapata mtihani mgumu, nimeona, kijana anampenda msichana, lakini msichana anaweka rangi kwenye midomo yake, kucha zake anaweka rangi, anachora na kalamu hapa kwenye nyusi kidogo, ukimtazama vizuri usoni utagundua ya kwamba ameweka kitu kingine juu ya uso wake.
Umempenda akiwa namna hiyo. Wakati ulipokuwa unamfuatilia hukumuuliza hayo maswali, leo ameingia ndani umemuoa, unamwambia sitaki hizo rangi! Hiyo ni kumwonea, maana ulimkuta akiwa hivyo, kama ulikuwa humtaki akiwa amejinakshi na rangi hizo, hukutakiwa kumfuatilia, wako wengine ambao watakuwa radhi na huyo anayejipaka rangi!
Kuna kijana alioa msichana, wamefika ndani wakaanza kugombana naye habari za nywele, mpaka akamrudisha kwao, nywele tu! Huyu dada kaenda katengeneza nywele staili fulani, yule kijana haitaki. Lakini alimkuta yule msichana anatengeneza nywele kwa staili hiyo, sasa kwa nini hivi vitu hawakutaka kuzungumza kabla ya kuamua kuoana?
Mimi ninataka nikusaidie upunguze ugomvi ndani ya ndoa utakayokuwa nayo; maana vitu ambavyo Mungu atawaletea vya kufanya pamoja kwenye ndoa ni vikubwa kuliko mnavyofikiri, kiasi ambacho hamhitaji kutumia muda wenu kushindania vitu vidogo vidogo ambavyo mlikuwa muwe mmekwisha kuvijadili kabla ya kuoana. Mna mambo muhimu sana ya kufanya, kiasi ambacho kuanza kushindana na kubishana juu ya vitu ambavyo mlitakiwa muwe mumeshavizungumza kabla ya kuoana; huko ni kutokuelewa utaratibu wa Mungu ulivyo juu ya kumpata mwenzi wa maisha.
JAMBO LA TISA: Uko Tayari kuoa au kuolewa lini, Maana yake ni Muda gani ambao ungetaka kuoa au kuolewa?
Utasikia mwingine anasema, siku Mungu atakapo nipa mume au mke, hii ni hatari sana! Biblia inasema kwenye kile kitabu cha Mhubiri.3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.
Kila kitu kilichoko chini ya mbingu kimeratibiwa, kwa lugha nyingine, ni kwamba kila mwanadamu ana kalenda yake, iko kalenda yako ya kuzaliwa, na ipo kalenda ya matukio na mipango mbalimbali, Mungu anaijua. Mungu anatangaza mwisho tangu mwanzo, anajua mwisho wa maisha yako wakati wewe unapozaliwa.
Katika mwanzo wa maisha yako, Mungu anakuwa amekwishajua mwisho wako; utakavyokuwa; na kama amekwishajua mwisho wako, maana yake ameshatembea kwenye maisha yako yote toka mwanzo mpaka alipofika mwisho, na alipokamilisha maisha yako akarudi mwanzo ndipo akakuongoza kuzaliwa.
Mungu anapokuacha uzaliwe duniani, hakika ujue kabisa ya kwamba amekwisha tembea na wewe katika maisha yako, amesharatibu mambo yako na yako hatua kwa hatua; kwa mfano, kitu gani utafanya, wapi utasoma, utasoma nini, utaolewa na nani au utaoa nani na itakuwa, lini, maisha yako yatakuwaje, utamtumikiaje, mpaka mwisho wako. Akiishafika mwisho wa maisha yako anarudi mwanzo, akishafika mwanzo anatangaza mwisho tangu mwanzo; kwa hiyo kuanzia hapo unapozaliwa ujue maisha yako yote yamesharatibiwa!
Ni vizuri ufahamu hii mistari itakusaidia, maana inakujengea msingi mzuri wa maisha hapa. Isaya.46:9-10 inasema, “Kumbukeni mambo ya zamani za kale maana mimi ni Mungu wala hapana mwingine, mimi ni Mungu wala hapana aliye kama mimi. Nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado, nikisema, shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote”.
Kwa lugha nyingine anatuambia ya kwamba, wewe unaona kila kitu ni kipya, unapoishi kila siku ni mpya, kila dakika inayokuja ni mpya, Mungu anasema hiyo safari unayopita, mimi nilikwishaipita tayari, nikafika mwisho wa maisha yako ndipo nikakuruhusu uzaliwe. Ulipokuwa unazaliwa nikatangaza mwisho wako tangu wakati unazaliwa.
Sasa mimi ninataka nikuambie kama Mungu anajua, na shauri lake anasema litasimama katika maisha yako, ili mapenzi yake ayatende katika maisha yako, unahitaji kuwa mwangalifu. Kwa sababu kuna mpango na saa ya Mungu ya kuoa au kuolewa, ipo!
Mungu anapokuletea mawazo ya kuoa au kuolewa, ni kwa ajili yakuimarisha maisha yako na wito wako na kazi na makusudi, ambayo ameyaweka hapa duniani. Atakuletea mtu atakaye imarisha wito wako, atakuletea mtu atakaye saidiana na wewe, uwe ni mwanamke au uwe ni mwanaume.
Mungu anapo kukutanisha na mtu wa kuoana naye ni kwa ajili ya kuimarisha nguvu zenu ili mtimize kusudi la Mungu. Kwa hiyo lazima anajua kuna saa huyu mvulana anahitaji mke, au huyu msichana anahitaji mume! Lakini watu wengi sana hawalifuatilii hili. Wakati sisi tunaoana na mke wangu tulikuwa bado vijana, tulioana hatujafikisha hata miaka thelathini, ninakumbuka nilikuwa na miaka 28. Tulijaliwa kuwapata watoto tungali bado vijana sana. Lakini tuna watoto ambao ni wakubwa kwa sasa. Tumefika kipindi ambacho tunaweza tukafuatilia masuala ya utumishi kwa namna ambayo haiwaumizi watoto wetu sana!
Maana watoto wakiwa wadogo wote, mimi ninakuambia kumtumikia Mungu ni kunakuwa kugumu sana, usije ukafikiri ni kurahisi. Maana unahitaji kuwa karibu nao; wanahitaji kusoma shule, wanahitaji kufanya vitu mbalimbali, wanahitaji kuwa na baba karibu, wanahitaji kuwa na mama karibu. Saa nyingine mnataka kusafiri nao; unaweza ukasafiri nao lakini usije ukafikiri ni kitu kirahisi.
Tulisafiri na Joshua (mtoto wetu wa nne) akiwa na wiki sita. Sijawahi kuona watu wakisafiri na watoto wao wakiwa wadogo namna hiyo, Joshua alikwenda kwenye huduma akiwa na wiki sita tu. Hatukuwa na namna ambavyo tungeweza kumwacha. Sasa unaweza ukaelewa akiwa na wiki sita; maana yake mama yake ana muda wa wiki sita tu tangu ajifungue na tulisafiri kwa gari, sio kwa ndege, bali kwa gari!
Tulisafiri masaa karibu kumi na mbili, tumebeba kila kitu, tumebeba mpaka unga wa kutengenezea uji, na beseni la kuogea, na maji. Huwezi kumwogeshea mtoto mchanga wa wiki sita maji yoyote tu, kwa hiyo tulibeba maji ya kumwogeshea. Huwezi kwenda ‘spidi’ unayotaka, ikifika saa yake ya kula lazima usimame! Ukifika kwenye hoteli huwezi kumlaza jinsi unavyotaka, lazima uingie kwanza uombe, uangalie yale mashuka yaliyoko halafu uombe, uangalie kile kitanda halafu uombe, uangalie kila kitu kule ndani halafu uombe!
Wewe ni mtumishi wa Mungu, ukienda na mtoto kienyeji kienyeji tu, ibilisi anaweza akamvamia na ukapata shida, na huduma yako yote uliyoiendea ikaharibika. Unaweza ukatamani saa nyingine usinge safiri naye. Lakini mnaposafiri pamoja, kumbuka ina gharama yake.
Lakini mambo haya unahitaji kufiri mapema, ili uweke kwenye agenda yako ya maombi ujue kabisa mpango wa Mungu ya kuwa unatakiwa kuoa au kuolewa lini. Ninajua kwa wengi kinakuwa kigumu hicho, maana wengine wametamani kuolewa jana, hawajapata wanaume, wengine wangetaka kuoa leo, lakini bado hawajapata msichana wa kuoa.
Wengine wanatamani kuolewa si kwa sababu mpango wa Mungu umefika wa kuolewa; ila ni kwa sababu wanaona muda wao wa kuolewa umefika, wengine wanaona umri umesogea. Mpango wa Mungu juu ya maisha yako, haubabaishwi na jinsi wewe unavyohesabu miaka, jirani zako wanavyohesabu miaka, ndugu zako wanavyohesabu miaka, au rafiki zako wanavyohesabu miaka.
Mungu anajua alichopanga kwa ajili yako, ana kalenda yako kabisa, na kila alichokichagua Mungu ndicho sahihi.
JAMBO LA KUMI: Uko Tayari kuzaa, kutunza na kulea watoto Wangapi?
Niliuliza vijana fulani ambao ndio wametoka tu kuoana, wanafurahia maisha yao, ghafla nikawauliza swali ambalo hawakutegemea, nikawauliza, “mna mpango wa nakuzaa watoto wangapi? Walinitazama wakasema, “Mungu anajua”. Nikawambia; “siyo hivyo! Mungu anajua lakini ninyi je?” “Wakasema hatujui”, nikawaambia hayo ndio makosa ya wengi waliomo katika ndoa.
Sasa ninakueleza hivi kwa sababu ni vitu ambavyo Mungu alisema na sisi mapema. Hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kuokoka ambaye sikujua ya kwamba atazaliwa, na hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kukuokoka ambaye sijajua wito wake. Na Mungu aliponyamaza na hakutuonyesha mtoto mwingine, hatukuona sababu ya sisi kutafuta mtoto mwingine. Wengine wanafikiri Mungu hana mipango ya uzazi (kasome biblia yako vizuri), Mungu ana utaratibu wa uzazi kwa kila ndoa anayoisimika.
Ni kitu ambacho unahitaji kuomba, ili Mungu akujulishe. Nimeona watu wakishindana ndani ya ndoa, baba anataka watoto wengi, mama hataki. Nimekuta ndoa nyingine mama anataka watoto wengi wamzunguke kama timu ya mpira lakini baba hataki. Na ugomvi mkali unatokea juu ya hili.
Mwingine anamzalisha mke wake kila mwaka (unaelewa maana ya kila mwaka?) si unaelewa mimba inakaa miezi tisa tumboni, kwa hiyo anaweza akazaa kila mwaka! Sasa umewahi kufikiri kila mwaka unazaa, kwa hiyo ikiwa uko kwenye ndoa miaka kumi basi una watoto kumi. Au mtu yuko kwenye ndoa miaka mitano, tayari ana watoto wanne na bado anaendelea kuzaa, hii ni sawa?
Nilikwenda mahali fulani kwa ajili ya huduma dada mmoja alikuwa anafurahia muujiza wake wa tumbo, jinsi ambavyo Mungu amemponya, akasema, “sasa nitakuwa tayari kuzaa mtoto mwingine”. Nikamuuliza, “una watoto wangapi sasa?” Akasema, “wanne”. Nikamwambia, “Na bado unahitaji mtoto mwingine”. Akasema, “ndio, ninataka mtoto mwingine”! Unajua kwa nini ninakueleza vitu vya namna hii, kwa sababu kila mtoto ana wajibu wake, ana mzigo wa kwake na anatunzwa kivyake!
Kadiri unavyozaa watoto wengi, ndivyo unavyozidi kuwa na wajibu mkubwa zaidi wa kulea. Watoto hawafanani, huwezi ukawalea kijumla. Watoto hawalelewi kwa namna hiyo. Kila mtoto ameitwa kivyake, ana mpango wake, ana njia yake, ana tabia yake na ana namna yake ya kutunzwa, hawafanani!
Mtoto anayezaliwa lazima umlee kwa uangalifu. Hujamfikisha mahali katika kumlea, tayari ameshakuja mwingine, unafikiri mchezo!
Hao watoto wawili hujawafikisha mahali katika kuwalea tayari ameshakuja mwingine, ni kitu kigumu hujawahi kuona! Huyu wa kwanza hapati tena ule umuhimu wake na nafasi yake, kwa sababu sasa anakimbiliwa huyu aliye mdogo; akija mwingine anakimbiliwa aliye mdogo zaidi, hao waliotangulia wanajikuta wanakua kivyao.
Watu wengi wanabaki kushangaa kwa nini watoto wengi waliozaliwa kwa kufuatana saa nyingine kwa karibu wanagombana. Ni kwa sababu huyu mkubwa anaona ameingiliwa na huyu mdogo, na huyu mdogo anaona kwamba huyu mkubwa ameshakuwa mkubwa, kwa hiyo mimi niliye mdogo ndiye mwenye haki zaidi. Ni ugomvi unaoweza ukaendelea mpaka wamekuwa watu wazima.
Mimi nimesoma masuala ya uchumi, sijasomea masuala ya kuhubiri. Si kwa sababu sikupenda kusomea kuhubiri, lakini hakuwa mpango wa Mungu wa kunilea namna hiyo katika wito. Kuna wengine Mungu anawapanga na kulea wito wao kwenye vyuo vya biblia; na ni mpango wa Mungu tu mzuri. Lakini Mungu alikuwa na mpango mwingine na mimi. Mimi katika chuo nilikwenda kusoma masuala ya uchumi.
Sasa, siku moja nchi hii ilitembelewa na wageni, wa kutoka Washington D.C, wa shirika la fedha ulimwenguni. Wale watu wakatuuliza maswali, hebu tuambieni mabadiliko ya uchumi yanayoendelea hapa nchini ninyi mnayaonaje.
Mama mmoja akanyoosha mkono, akasema, “Tunaelewa umuhimu wa mabadiliko mengine yanapotokea katika uchumi wa nchi, kwa sababu ya mazingira tunayoyaona hasa tunapoona vitu vingine havifanyi kazi. Kwa hiyo kuna umuhimu wa kubadilisha sera zingine ili mambo yaende sawasawa.
Lakini tatizo tulilonalo, ni kwamba maandalizi ya kutuandaa sisi kama watanzania ya kwamba kuna mabadiliko yanakuja, hayo maandalizi hayajafanyika ya kutosha”. Wakasema, “mama tupe mfano”. Akasema “kwa mfano, tunatakiwa kuchangia masuala ya afya, tunatakiwa kuchangia masuala ya elimu, kama tungejua kwa mfano, miaka mitano au sita kabla, kwamba miaka sita ijayo au miaka kumi ijayo, ya kuwa pamoja na kwamba sasa elimu ni bure, afya ni bure, iko siku mtahitaji kutoa pesa zenu mfukoni ili kulipia gharama hizi tungekuwa waangalifu tunazaa watoto wangapi.”
Nikagundua mara moja kwamba huyu mtu wazo lake lilikuwa ni zuri kabisa. Kwa sababu kwa watanzania wengi inapofika mtoto anazaliwa walijua anayewajibika kumpeleka huyo mtoto shule ni serikali, anayewajibika kumlipia gharama za hospitali ni serikali! Wewe utazaaje ili serikali ikutunzie mtoto? Lazima na wewe uwe na bajeti yako!
Unajua biblia haisemi serikali leeni watoto, inaasema enyi wakina baba leeni watoto. Soma Waefeso 6:4 “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana”. Sasa pale serikali itakapokusaidia wacha ikusaidie, lakini usikae unajiambia ya kuwa mimi nimezaa watoto kumi na tatu, lazima waende shule bure, lazima waende kwenye hospitali bure. Nani anayegharamia hizo huduma, unafikiri ni za bure? Hakuna! Wewe unaona huduma hizo ni bure, lakini yuko mtu ametoa pesa za kugharamia hizo huduma toka mahali fulani.
Nakumbuka wakati fulani nlikuwa Zimbabwe, baba mmoja aliyekuwa na cheo kikubwa tu kwenye makanisa ya kule Zimbabwe, tulikuwa tunazungumza naye siku moja juu ya masuala ya kusomesha watoto. Alisema wakati mmoja alikwenda Ujerumani kwenda kutafuta watu wa kuwasomesha watoto wake.
Yule mzungu ambaye alikuwa anazungumza naye, akaamuuliza, “ndugu una watoto wangapi, akasema sita”. Akasema, “unajua mimi nina watoto wangapi.” Akasema, “sijui”. Akasema watoto wawili”. Akasema, “unajua ni kwa nini hatutaki kuzaa watoto wengi, usije ukafikiri tunachukia watoto, hasha ila ni kwa sababu ya gharama, za kuwatunza zilivyo kubwa”.
Tunataka angalao kila mtoto atunzwe vizuri na aende shule nzuri, wakiishakuwa wengi inakuwa si rahisi kuwagharamia wote ipasavyo, na inabidi ugawe ulichonacho kidogo kidogo. Wanaishia wote shule ya msingi, kwa sababu huna hela ya kuwapeleka sekondari. Akasema, “sasa ninyi waafrika mambo yenu hayako sawa, wewe unaona mimi nimezaa kidogo nimejinyima kwa ajili ya watoto wangu wasome vizuri, sasa unataka fedha ya kwangu nikusomeshee watoto wa kwako ambao wewe umezaa bila kufikiria jambo la gharama ya kuwatunza wakiishazaliwa?”
Aliambiwa kitu cha kweli usoni na mzungu! Unaweza ukafikiri alikuwa anamtukana, lakini alikuwa anamweleza kitu cha ukweli; watu wengi sana hawafikiri hiki kitu. Wale wazee wa zamani walikuwa wakizaa kwa mahesabu huku nyuma. Akizaa watoto wa kike wengi ana hesabu ng’ombe atakazopata watakapoolewa, usije ukafikiri ana hesabu gharama, bali ana hesabu ng’ombe atakazopata! Watoto wa kike kwake ni mradi. Akizaa watoto wa kiume anajua amepata nguvu kazi ya kulima mashamba, walikuwa wana mahesabu yao.
Lakini sasa hivi lazima ukae ufikiri kwa namna nyingine, sikuambii ya kwamba kuwa na watoto wengi ni kitu kibaya, ni uamuzi wako! Kama unataka kwenda na mstari unaohimiza mkaongezeke mkaijaze nchi (Mwanzo 1:28) hakuna shida! Unaweza ukaendelea na wewe ukawa kwenye kuijaza nchi, lakini usikazane kuijaza nchi halafu unataka wengine wakusaidie kulea watoto hao, hiyo sasa sio sawa!
Mimi sijui kwa upande wako, na sijui kwa upande wa wazazi wako, lakini ninakueleza ili baadaye uwe mzazi mzuri, ni vitu unahitaji kufikiri mapema. Niliwaambia watoto wangu siku moja, nikawaambia sikiliza, tumejiwekea maamuzi ndani ya hii nyumba mimi na mama yenu, ya kwamba ni wajibu wetu kuwasomesha mpaka chuo kikuu ili angalau kila mmoja awe na shahada ya kwanza, huo ni wajibu wetu.
Baada ya shahada ya kwanza ukitaka kuendelea Mungu akubariki. Mungu akitupa nafasi ya kukusaidia kuendelea zaidi ya shahada ya kwanza tutakusaidia. Lakini tumemwomba Mungu atusaidie, kila mtu lazima afike chuo kikuu. Unajua kama usipoweka malengo ya namna hii, hata matumizi yako na bajeti yako haviwezi kukaa sawa. Ndio maana ninakuambia lazima umwombe Mungu akusaidie, usije ukafikiri kusomesha watoto ni kitu rahisi.
Ninyi mnajua ambao mko shule, wengine wameshindwa kuendelea na shule kwa sababu wazazi wameshindwa kutoa karo za shule, na sio kwa sababu wanafunzi hawataki kuendelea na shule, lakini ni kwa sababu hakuna fedha za kuwasomesha.
Nilimuuliza msichana mmoja katika mkoa mmoja wakati nilipokuwa huko kwa huduma, nikamuuliza “umemaliza darasa la ngapi”. Akasema, “kidato cha sita”. Nikamwambia, “sasa kwa nini hutaki kuendelea na shule?” Akanitazama usoni, halafu akasema, “sithubutu hata kumwambia baba anisomeshe zaidi maana ninawaangalia wadogo zangu huku nyuma walivyo na ninaangalia na hali ya baba yangu aliyonayo kifedha, amenisaidia nimefika kidato cha sita, sasa nikifikiria wadogo zangu ambao bado wako shule za msingi, naona wacha na wao basi wasogee sogee angalau wafike sekondari na wao kama mimi. Kwa hiyo mimi nimenyamaza kimya”.
Huyu msichana amemaliza kidato cha sita anataka kuendelea na masomo, lakini hawezi kuendelea kusoma kwa sababu anaangalia hali ya wazazi wake ilivyo, anajua kabisa angalau na wadogo zake na wao wasome, lakini sio kwamba anataka kuishia kidato cha sita.
JAMBO LA KUMI NA MOJA: Uko Tayari kuishi katika hiyo ndoa kwa Muda Gani?
Sasa ninakupa siri hapa ikusaidie, Kama umekaribia karibia kuoa au kuolewa, na hujawahi kujiuliza maswali ya namna hii, basi Mungu anakuweka mahali pazuri kwa kukupa nafasi ya kusoma kitabu hiki. Labda nikuambie kitu cha namna hii kitakusaidia, kabla sijakupa mistari mingine kwenye biblia, ni hivi: Hakuna sababu ya kuolewa na kijana ambaye atakufa baada mwezi mmoja. Au hakuna sababu ya kuoa msichana atakayekufa muda si mrefu baada ya arusi yenu.
Kwa nini uolewe leo uwe mjane baada ya miezi miwili? Na ukiishaolewa umekwisha badilisha kabisa hali yako na ya mume wako; akiisha kufa wewe sio msichana tena, utaitwa mjane, hata kama umri wako ni mdogo. Tulienda mahali fulani tukasema tunaomba wajane tuwaombee, tulishangaa kuona ya kuwa robo tatu yao walikuwa ni wasichana. Ungeambiwa wameolewa ungekataa, lakini wamefiwa bado wana umri mdogo.
Sasa mimi ninataka nikuulize swali, kwa nini unataka uolewe, halafu mume wako afe baada ya miezi miwili au unataka uoe mke wako afe baada ya mwezi mmoja, au baada ya mwaka? Hakuna kitu kinachosumbua kama hiki. Ngoja nikueleze hili tena ya kuwa ndoa ya pili sio ndoa ya kwanza. Ndoa ya kwanza ina utofauti wake, na ndoa ya pili ina utofauti wake.
Ikiwa unataka kuishi muda mrefu na mwenzi wako wa ndoa unahitaji:
1: Kuwa mwangalifu kutii ile mistari ilioko kwenye biblia inayozungumzia juu ya muda wa mtu kuishi. Kwa mfano: Waefeso 6:1-3 inasema; “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, upate heri, ukae siku nyingi katika dunia”
Kwa hiyo angalia uhusiano wako na wazazi wako kama bado wako hai. Lakini pia chunguza uhusiano wa huyo anayetaka kukuoa au anayetaka umuoe, na wazazi wake, kama bado wako hai.
2: Omba Mungu akupe maisha marefu na huyo mwenzako hata kabla hamjaamua kuoana. Ili kama kuna mmoja wenu hataishi muda mrefu basi Mungu awaarifu na kuwaongoza cha kufanya.
Mwingine anataka aingie kwenye ndoa kwa kubahatisha au kwa majaribio. Maana yake ndani ya nafsi yake anajiweka tayari kuachana na mwenzi wake kama anaona mambo ya ndoa yake hayaendi alivyotarajia. Mtu wa namna hii hataweza kuwa mvumilivu na mwepesi wa kutafuta suluhisho kukitokea tatizo katika ndoa yake.
Uamuzi wa kuoa au kuolewa unamtaka mtu aingie katika ndoa asilimia mia moja. Ikiwa hautakuwa tayari kuingia kwenye ndoa kwa asilimia mia moja, tafadhali usiamue kuoa au kuolewa. Utampotezea tu mwenzako muda maana hakuna ndoa isio na matatizo. Lakini pia hakuna tatizo ambalo Mungu hawezi kulitatua. Lakini, je, uko tayari kushirikiana na Mungu katika ndoa kwa kiwango cha asilimia ngapi?.
MWISHO!

Barikiwa sana Mtumishi, mafundisho mazuri sana.
JibuFutaMungu akubariki.
Asante kwa mafundisho haya yamenipa mwanga zaidi.
JibuFutaAsante kwa mafundisho haya yamenipa mwanga zaidi.
JibuFutaNamshukuru Mungu amenipa neema ya kusoma mafundisho haya, hakika yamenijenga.
JibuFutaAsante Yesu..mafundisho haya yamenipa mwanga sana🙏
JibuFutaAmen Barikiwa san Mtumishi wa Mungu
JibuFutaHongera Sanaa mwalimu, mtumishi, hakika kazi yako si bure,usichoke kwani tunazidi kufahamu mambo yaliyofichika
JibuFuta