Ijumaa, 12 Aprili 2013

Somo la malango ni somo pana, zuri sana lakini halifundishwi makanisani ama kwa sababu wachungaji wengi hawalipi umuhimu wa hali ya juu au wanadharau kuwa halina madhara(effect whether negative or positive) kwa waumini wao au jamii kwa ujumla wake. Lakini nataka kukuhakikishia kuwa watu wengi sana waliookoka au wakristo wa kawaida wamebanwa sana na malango kiasi kwamba kila wanachokifanya hakisongi mbele.

Maana rahisi ya malango ni maeneo ni maeneo mbalimbali yaliyopo kwenye ulimwengu wa kimwili yanayotumiwa na ulimwengu wa kiroho katika kuingiza mambo ya falme hizo kwenye ulimwengu wa kimwili. Haya ni maeneo ambayo Mungu aliyaumba mwenyewe na kwa sababu shetani alikuwa malaika mkuu wakati huo, anayajua yote wakati sisi wanadamu hatuyajui, na hatuyajui kwa sababu ni wahubiri wachache sana wanahubiri na kueleza juu ya malango. Yapo malango ya aina nyingi sana, na ili mawasiliano kupitia malango haya yaweze kuwa na ufanisi, kila falme yaani ufalme wa nuru(Mungu) na ufalme wa giza (shetani) lazima ufuate sheria zake ili kuweza kudhibiti malango hayo.

AINA MBALIMBALI ZA MALANGO.
Kama nilivyosema hapo juu zipo aina mbalimbali na nyingi sana za malango, hizi zifuatazo ni baadhi tu:

1.Taifa la Israel ni lango kuu la Mungu kupitishia baraka zake kwa dunia nzima.Baraka hizi zinaweza kuwa za kiuchumi, kijamii au kisiasa. Kwa nini tunasema Israel kama taifa ni malango kwa sababu ni mzaliwa wa kwanza wa Mungu (Kutoka 4:22-23).

2.Adam wa kwanza alikuwa lango kabla na baada ya kutenda dhambi.Hapo nina maana kwamba kabla ya dhambi alikuwa lango lililopitisha mambo ya ufalme wa Mungu, lakini baada ya kutenda dhambi likawa lango la kupitisha mambo ya ufalme wa giza(dhambi) ndio sababu maandiko yanasema kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni hata mauti ikawafikilia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi kwa huyo mtu mmoja(Rumi 5:12-14).

3. Malango ya wazaliwa wa kwanza. Hili ndilo lango pana sana na somo lake ni pana mno, nadhani wengi waliofuatiliaji wa semina za Mwl. C. Mwakasege wataelewa nini ninachokizungumza kuhusu upana wa malango ya mzaliwa wa kwanza. Kwa kifupi ni kwamba ni kwamba mzaliwa wa kwanza wa binadamu ni lango. Kwa upande wa binadamu amegawanyika katika sehemu mbili, mzaliwa wa kwanza kicheo na mzaliwa wa kwanza kwa haki. Kule tu kuzaliwa wa kwanza hicho ni cheo, lakini si lazima wazaliwa wote wa kwanza kuwa pia wazaliwa wa kwanza kwa haki. Kwa kifupi ni kwamba mzaliwa wa kwanza kwa cheo hupitisha nasaba (geneology) za familia yake na mzaliwa wa kwanza kwa haki hupitisha baraka mbalimbali za Mungu kwa ajili yake mwenyewe na wale wote wanaomhusu. Hivyo familia moja inaweza kuwa na mzaliwa wa kwanza kicheo na pia akawa mzaliwa wa kwanza kwa haki, lakini vilevile Mungu anaweza kumnyang’anya mzaliwa wa kwanza wa cheo haki ya kuwa mzaliwa wa kwanza wa haki na kumpa mtoto mwingine yeyote yule ndani ya hiyo familia ili aweze kupitisha baraka zake kwenye hiyo familia (Waebrania 12:16-17 Esau aliuza haki ya mzaliwa wa kwanza alipotaka kurithi baraka haikuwezekana kwa sababu hakutubu). Mtu aliyebaki kuwa mzaliwa wa kwanza wa cheo na wa haki ni baba yetu wa imani mzee Ibrahimu. Lakini mtoto wake wa kwanza Ishmael alibaki kuwa mzaliwa wa kwanza kwa cheo, wakati Isaka akawa mzaliwa wa kwanza wa haki na ndiko baraka na agano la Mungu lilikopitia (ingawa Ishmael naye alibarikiwa lakini ilikuwa nje ya agano la Mungu). Kwa hiyo ni muhimu sana kujifunza kukaa ndani ya agano la Mungu, maana baraka ndani ya agano la Mungu ni kubwa na nyingi sana, sio kwa ajili yako tu, bali pia kwa ajili ya jamii nzima.

Lakini pia kwenye hili lango la mzaliwa wa kwanza ni muhimu sana kujua kuwa kila anayeokoka na kumpokea Bwana Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake anafanyika au anakuwa mzaliwa wa kwanza, kwa maana hiyo familia moja inaweza kuwa na malango mengi ya wazaliwa wa kwanza, na lazima yote yawekewe ulinzi imara ili yasije yakatekwa na adui.

4. Yesu Kristo ni lango pia kwa sababu ni mzaliwa wa kwanza (Waebrania 1:5-6) na tena ni Adamu wa Mwisho ambaye kwa kukorofisha kwa yule Adamu wa Kwanza ilibidi lazima aje Adamu wa Mwisho ili kila anayemwamini apate kurithi baraka na ahadi zote za Mungu (2 Korintho 1:20).

5. Malango ya kuzimu (Mathayo 16:18)

6. Malango ya haki(Zaburi 118:19-20)

7. Sifa ya mtu, nchi, mji au kitu kingine chochote ni lango kwa sababu linaweza kuingiza mambo ya Mungu au mambo ya shetani. Kwa hiyo ni muhimu sana kwa wapendwa kujua sifa ya miji yao wanakoishi au kampuni/mashirika wanakofanyia kazi ili kuyadhibiti malango hayo, hata mahali wanapoabudu, wakizembea kidogo tu shetani anadhibiti mahali hapo kama ilivyokuwa kwenye kanisa la Pergamo katika Ufunuo wa Yohana 2:12-13. Hawa ndugu walijenga kanisa mahali ambapo shetani alikuwa amesimika kiti cha enzi. Biblia inaposema kiti cha enzi maana yake ni utawala yaani shetani ndiye alikuwa mtawala wa eneo hilo yaani alikuwa amedhibiti malango ya Pergamo.

8.Hekima ni lango pia. Ukitaka kujua kuwa hekima ni lango soma habari za mfalme Suleimani. Kwa sababu ya hekima aliyopewa na Mungu aliishia kuwa na wake 700 na masuria 300, na wote hao walikuja kwake kutaka kuona hekima aliyokuwa nayo, lakini hawakwenda kwake bure, walienda na miungu yao kiasi kwamba mwisho wa maisha ya Suleimani, moyo wake ukashindwa kumwabudu Mungu wa kweli.Hivyo mpendwa mtu wa Mungu, ukianza kuambiwa na watu una hekima sana basi dhibiti lango hilo kwa sababu adui naye analitaka ili apitishe mambo yake.

9. Maeneo mbalimbali katika miji na vijiji pia ni malango. Kwa mfano iwe ni vijijini au mijini mahali njia zinapokutana(makutano ya njia au roundabouts) ni malango hivyo wapendwa lazima wayadhibiti.Barabara kubwa ziingiazo mijini,n.k.Elimu na mafundisho mbalimbali nayo ni malango kwani ni moja ya mihili ya serikali za ulimwengu wa roho katika kusaidia utekelezaji wa sera za serikali hizo(kumbuka neno rahisi la ufalme ni serikali inayotawaliwa kifalme) kwa kuiandaa jamii kukubaliana na sera za serikali husika.

Kwa hiyo ndugu Atugonza vita vya kiroho havipiganwi bila eneo,lazima pawe na maeneo la maalum nayo huitwa malango, hebu soma kwa makini Waamuzi 5:8 inazungumzia vita ya miungu hupiganwa malangoni.

Hii ni kwa kifupi sana Roho Mtakatifu awafunulie zaidi Amen

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni