Jumatatu, 15 Aprili 2013

UONGOZI WA KIROHO


SEHEMU I

  1. UTANGULIZI
Uongozi na Kiongozi. Nini tofauti yake?.

- Uongozi ni tendo la kuongoza, hali ya kutangulia mbele au kuelekeza watu njia au mwelekeo wa kuendea jambo au kufikia malengo fulani.

- Kiongozi ni mtu yule ajuaye njia au mwelekeo wa jambo hilo au malengo hayo na ana uwezo wa kuwatangulia na kuwavuta wengine wamfuate.

Musa – Kut. 10:25,26, Kut. 13:21,22,
Yuda – Mwa. 46:28,
Yesu – Yoh. 14:6, 10:2-4,
Paulo - 1Kor. 11:1, 4:16.

Kwa nini viongozi wanahitajika?

Hitaji kubwa la nyakati zote katika watu wa kada zote, jamaa, taifa na mataifa, taasisi na mashirika ya dini ni kupata viongozi wenye sifa na uwezo wa kuwaongoza. Wenye uwezo na hekima katika kuwaunganisha watu ili kuwafanya kuwa wamoja katika kutumia karama, vipawa na talanta au rasilimali walizo nazo kwa manufaa ya maendeleo yao, pia waweze kufikia na kulikamilisha jambo au malengo na mipango yao waliyokusudia. Viongozi wanajua wanalopaswa kulifanya na wana uwezo wa kuwachukua watu mbele zaidi ya pale walipo sasa.

  1. TOFAUTI YA KIONGOZI WA KIROHO NA WA KIDUNIA

Uongozi wa kiroho na ule wa kidunia unaweza ukafanana katika baadhi ya mambo fulani tu, lakini ukatofautiana sana na kwa kiasi kikubwa katika mambo ya kimsingi. Kwa mfano katika mambo yafuatayo:-

i). Hitaji na maandalio ya kiongozi: Mungu huandaa na kuweka Viongozi.

1Sam. 16:3,7 “Umwite Yese, nami nitakuonyesha utakayotenda, nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako…Bwana akamwambia Samweli, usimtazame uso wake wala erefu wa kimo chake, .. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo, maana binadamu huangalia sura ya mtu, bali Bwana huangalia moyo”. (Eze. 16:1-5, 1Tim. 3:1,15)

Yer. 3:15. “Nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na ufahamu”.

Mat. 9:38 “Basi, mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake”.

ii). Nia ya ndani ya Kiongozi:

- Kwa nini wewe ni kiongozi au unataka kuwa kiongozi?
Zipo nia mbalimbali kama vile kutaka mamlaka, sifa, kuheshimiwa, utukufu, kutosheka, kushika hatamu, utajiri, kutambulika, kiburi, nafasi nzuri nk. Ambazo hizo ni nia za viongozi wa kidunia.

- Na pia mtu anaweza kuwa kiongozi kwa nia ya kutaka kuyafanya mapenzi ya Mungu.
- Flp. 2:5,13 “Iweni na nia iyohiyo ndani yenu ambayo iliyokuwamo pia ndani ya Kristo Yesu.. maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”

- Uongozi wa kidunia unadhihirishwa katika nia binafsi katika kupata mafao yenye kumnufaisha yeye na familia yake, kupata malupulupu mazuri yenye kuinua heshima yake bila kujali wengine kama wanaumia au la. Hivyo watu wanapigania kuwa viongozi kwa nia ya cheo, na kuona umuhimu zaidi kuliko huduma yenyewe itakayotolewa au utendaji / uongozi wa kazi yake kwa watu.

- Uongozi wa kiroho, Mungu anasema “Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno, bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mabo ya wengine.” (Flp. 2:3,4)

iii). Kutaka mapenzi ya Mungu:

- Rum. 12:2. “…msiifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe na kufanywa upya nia zenu na kujua hakika mapenzi ya Mungu.” (Efe. 5:17)

- 1Tim.3:1. “Ni Neno la kuaminiwa, mtu atakaye kazi ya askofu, atamani kazi njema”. Tunaona Mungu hamkatai mtu yeyote kuhitaji kuwa kiongozi, anatamani kazi njema. Lakini nini hasa nia yake ya moyoni? Hilo ndilo litakalombainisha kama atakuwa kiongozi wa kiroho au wa kidunia.

- Kiongozi wa kiroho, yeye ni kiungo au mpatanishi kati ya Mungu na watu anaowaongoza.

Mfano:

Musa: Kut. 19:9, 24:3. “Bwana akamwambia Musa, Mimi naja kwako katika wingu zito, ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia Bwana hayo maneno ya watu. …. Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote, watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyasema Bwana tutayatenda.”

Yesu: Yoh. 8:26-30. “Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu, lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake ndiyo ninenayo katika ulimwengu… sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha, ndivyo ninenavyo. Naye aaliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu, kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo. Na alipokuwa akisema hayo wengi wakamwamini.”

Paulo: 2Kor. 5:18-20. “Lakini vyote vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho… ametia ndani yetu neno la upatanisho… Basi tu kwa ajili ya Kristo…twawaomba ninyi mpatanishwe na Mungu.”







SEHEMU II


3. UMUHIMU WA UONGOZI

Uongozi tunaona ni muhimu sana mbele za Mungu na kwa watu pia. Uongozi ni kipawa cha Mungu kwa wanadamu ili wakae katika amani na matumaini. Bila uongozi watu hukosa mwelekeo na amani, hivyo kusababisha watu kufikia hatua ya kufarakana, kutawanyika kukosa mwelekeo, kila mtu kwenda au kutenda lile analoona linamfaa yeye machoni pake. Kwa sababu hiyo Mungu ameweka uongozi ili watu wapate mwelekeo, amani na matumani katika kuyatimiza mapenzi yake duniani. Tunasoma katika Biblia kuwa:

Amu. 21:25: “Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli, kila mtu allifanya yaliyokuwa mema machoni pake mwenyewe.”

Zek. 13:7: “…Mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika..”

Hes. 27:15-23: “Musa akanena na Bwana akisema; Bwana Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano, atakayetoka mbele yao, atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa Bwana usiwe kama kondoo wasio na mchungaji.”

Efe. 4:11-13: “Naye alitoa wengine kuwa Manabii, na wengine kuwa Mitume, na wengine kuwa Wainjilisti, na wengine kuwa Wachungaji na Waalimu. Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe, hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani, na kumfahamu sana mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo ha utimilifu wa Kristo. Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, na hila ya watu, kwa ujanja tukizifuata jia za udanganyifu”.


4. SURA YA UONGOZI WA KIROHO

Mambo matatu yanayotakiwa kuonekana ndani ya uongozi wa kiroho ni kama yafuatayo:-

i) Utumishi
ii) Uchungaji
iii) Uwakili

i) UTUMISHI

Mk. 10:45, Lk. 22:24-27, Mat. 20:26-28, Yoh. 13:17.

a) Je, wewe ni kiongozi wa aina gani?

- Mimi ni kiongozi ninayeongoza.
- Mimi ni mtumishi ninayetumika.
- Mimi ni kiongozi mtumishi.
- Mimi ni mtumishi kiongozi.

b) Mtumishi kiongozi - hii ni filosofia inayowasaidia watu kuwa na dhana ya utumishi; na baadaye kuweza kuongoza kwa nia kuwatumikia watu, shirika au kanisa. Mtumishi kiongozi anaweza asiwe na cheo chochote kanisani na bado akawa tegemeo la watu wengi, kutoka kwake, watu wanapokea hazina njema kutoka kwake kwa jinsi anavyowatumikia na kuwaongoza kwa namna moja au nyingine.

Neno la Mungu linatuonyesha maneno ya msingi na yenye hekima katika utumishi kama yafuatayo:-

Lk. 22:26,27: “Lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo, na mwenye kuongoza kama yule atumikaye..Lakini mimi (Yesu) kati yenu ni kama atumikaye”.

Mat. 20:26-28: “..Bali mtu yeyote atakaye kuwa mkubwa kwenu na awe mtumishi wa wote; na mtu atakayekuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi”.

1Pet. 5:2,3: “Wala si kama wajifanyao mabwana katika mitaa yao; bali kwa kujifanya kielelezo kwa lile kundi”.

c) Tabia ya Mtumishi kiongozi:-
- Mnyenyekevu. (Mat. 10:24, 2Tim. 2:25)
- Ana bidii si mvivu. (Mat. 24:45-47)
- Ana uwezo wa kufundisha. (2Tim. 2:24)
- Mvumilivu. (2Tim. 4:2)
- Mtii. (Ef. 6:5,6, Tito 2:9)
- Amejitoa. (2Sam. 15:21)
- Mwangalifu. (Lk. 12:35,36)
- Mwaminifu. (1Sam. 22:14)
- Amejaa Roho Mtakatifu. (Mdo. 2:16,18)

ii) UCHUNGAJI
Zab. 23, Yoh. 10:11, 21:15-17, 1Pet. 5:2-3.

a) Kiini cha uchungaji
- Neno mchungaji lilitumika sawa na mchungaji wa kondoo, n’gombe au mifugo mingine. (Yer. 6:3, Mat. 8:33)
- Mchungaji hukaa na kondoo na kazi yake muhimu ni kuwa na kondoo hizo.
- Kondoo ndiyo wanampa kazi ya kuwa mchungaji, hivyo mchungaji ni mtumishi wa kondoo.

b) Sifa ya mchungaji
- Mchungaji anawajua kondoo wake kwa majina. (Yoh. 10:3,14,27). Sawa na Haruni juu ya wana wa Israeli. (Kut. 28:9,10,12,29)
- Mchungaji yuko pamoja na kondoo au anapatikana na ni rahisi kuingilika. (Lk. 22:27)
- Mchungaji anatangulia mbele kuwaonyesha kondoo mahali pa malisho, majani na maji. (Zab. 23:1,2)
- Mjasiri na yuko tayari kujitoa kwa ajili ya kondoo. (Yoh. 10:10-18)
- Anawaongoza na kuwaelekeza kwa upole kwa fimbo ya kichungaji. (Zab. 23:4, Ufu. 21:15)

c) Ili kutimiza wajibu wake kwa kondoo
Mchungaji anapaswa kujua mambo matatu.
- Kwamba ameitwa na Mungu. (Yoh. 15:16)
- Kufahamu chanzo cha nguvu zake. (Kol. 1:11,29, Zek. 4:6)
- Kufahamu mambo aliyoitiwa kufanya, na hata jinsi ya kuyapatia vipao mbele. (Yoh. 10:4)

Mambo hayo humfanya mchungaji kuwa na maono, malengo na mipango katika kazi yake. (Kol. 1:10, Efe. 4:1)

d) Mchungaji anapaswa kuhakikisha kuwa kundi lake
- Linaongezeka kiidadi. (Mdo. 2:47, 41, 6:7)
- Linakua kiroho. (Mdo. 2:42, 2Kor. 2:14, Kol. 1:10)
- Linamwabudu Mungu katika Roho na kweli. (Yoh. 4:24, 2Kor. 4:2)
- Linahifadhi umoja na ushirika katika mwili wa Kristo. (Fil. 1:27, Efe. 4:1-6)
- Linaushuhudia ulimwengu habari njema na kuwaleta kwa Kristo. (Mdo. 5:42, 6:7)
- Linapata ulinzi au usalama na amani. (Mdo. 20:28-31)

e) Tahadhali za mchungaji kama kuhani wa Mungu ni kuona kuwa:-
- Katika uongozi wake asiwe sababisho la kundi kutawanyika.
- Yer. 23:1,2: “Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema Bwana… Mungu asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu. Mmetawanya kundi langu na kuwafukuza, wala hamkuenda kuwatazama, angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana”.

- Eze. 34:2-5,10: “Ole wao wachungaji wanaojilisha wenyewe, je haimpasi mchungaji kulisha kondoo? Mnawala walionona, mmejivika manyoya, mnawachinja walionona lakini hamwalishi kondoo. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea, bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala. Nao wakatawanyika kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wakawa chakula cha mbwa-mwitu, wakatawanyika.”

- Hapotoshi mafundisho ya kweli, yaani hafundishi kwa nia ya kulidanganya kundi kwa manufaa yake binafsi.

- Eze. 22:26,30: “Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa siku zote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu viichafu na vitu visafi, nao wamefumba macho yao.. Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.”

- Tito 2:7,8: “Katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa..” (Eze. 13:1-7, Isa. 10:1-3, Yer. 14:14)

- Anatoa malisho kwa kundi kama Mungu anavyokusudia na kwa wakati unaokubalika.

- Yer. 23:22: “Lakini kama wangalisimama katika baraza yangu,ndipo wangaliwasikizisha watu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya na uovu wa matendo yao.”

- Mat. 24:45,46: “Ni nani basi, mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo”.

- 2Tim. 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli”. (2Tim. 4:5)

- Kwa kufanikisha haya mchungaji lazima anazingatie Maombi na kusoma Neno la Mungu kila wakati.

- Mat. 17:20,21: “Kwa maana amini nawaambia, mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu. Ondoka hapa uende kule, nao utaondoka, wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga”.

- Yoh. 15:7: “Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu. Ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” (Fil. 4:6, 1The. 5:17, Kol. 3:16, Yoh. 17:14-17)

iii) UWAKILI

Mat. 25:14, 1Kor. 4:1,2.

- Katika Agano jipya, wakili alikuwa ni mtu aliyeaminiwa na bwana wake; na hivyo alipewa mafao na mamlaka na pia alikuwa na wajibu na uajibikaji kwa kazi yake. (Lk. 12:42-43)

- Wakili alipaswa kuangalia vipawa katika maisha ya wale anaowangoza ili avitumie vizuri na kuzalisha. (2Tim. 1:14, 1Tim. 1:18-20)

- Wakili anapaswa kuhesabu rasilimali zote alizonazo, kama vile, watu, fedha, vifaa na kwa neema ya Mungu kuweza kupanga na kuvitumia ipasavyo.

- Wakili anapaswa kuwa mkweli (honesty), mwenye msimamo mwema (integrity) na muwazi (transparency). (Yoh. 8:12)

- Mtu mwaminifu na mwenye kupandishwa daraja kwa uaminifu wake. (Mat. 25:21) ”Bwana wake akamwambia,Vema mtumwa mwema na uaminifu, ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi…”

1Kor. 4:1,2: “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu” (Mat. 24:45-47)







SEHEMU III




5. MAADILI YA KIONGOZI WA KIROHO

Maadili ni jambo linaloweza kutenganisha sifa za uongozi katika muonekano wake kati ya uongozi wa kiroho, na wale uongozi wa kidunia. Maadili yapo hasa kuonyesha msimamo katika usafi wa maisha na haki.


Mtume Paulo katika 1Kor. 10:23, 6:12 anasema:
Vitu vyote ni halali, bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo. …. lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu chochote.”

Vipi yale mambo yanayokupa msukumo zaidi na yale unayoyapendelea kuyafanya, licha ya kuwa unayofanya yanamkosea Mungu? Na pengine yamekuwa kikwazo hata kwa wale unaowaongoza! Unajionaje mbele za Mungu, je, ni sawa au si sawa?

- Katika waraka wa kwanza kwa Timotheo 3:2-12. Neno la Mungu limeeleza maadili ya msingi kwa kiongozi wa kiroho ya kuwa anapaswa awe mtu wa: - kutokulaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtaratibu, mkarimu, mwenye kujua kufundisha, si mlevi, si mpiga watu, si mtu wa majadiliano, si mpenda fedha, mwenye kusimamia nyumba yake, si mchanga kiroho, mwenye kushuhudiwa na walio nje. Si mwenye kauli mbili, asiyetamani fedha ya aibu. (Tito 1:6,7)

- Maadili yanatusaidia kuishi maisha ya mfano au kielelezo.
Katika Tito 1:8,9 tunasoma kiongozi awe “Mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake, akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima na kuwashinda wenye kupinga.”

(2Thes. 3:9, 1Tim. 4:12, 1Sam. 12:2-5)
- Unayoyafanya yatageuza watu zaidi ya yale unayoyasema.
- Unavyoishi itasaidia kukazia mafundisho yako au pia kuyaondoa kabisa mioyoni mwa watu wanaokutazama.
- Kumbuka kuwa watu hujifunza zaidi kwa kuona, kisha kwa kusikia na kwa kiasi kidogo kwa yale mengineyo.
- Maadili bora ni uamuzi na misimamo inayoweza kumfanya mtu binafsi au jamii iweze kuishi maisha ya haki, utaratibu, na usafi.

Mfano wa watu wawili:-

Sauli

Yeye aliitwa na Mungu kuwa mfalme, alipakwa mafuta na kutumiwa na Mungu; lakini….
(1Sam. 13:13,14)
- Alikuwa mtu wa kutenda bila kufikiri, aliweza kutoa sadaka kinyume na utaratibu wa Mungu.
Alikuwa mtu wa kutumia mabavu, kiburi, kutotii na kupenda umaarufu.
(1Sam. 15:12-26)
Mwisho wa yote, alianguka na kukataliwa na Mungu. Alijiwekea maadili mabaya, ambayo hayakumpa Mungu utukufu.
Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli kusema, Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme, maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya niliyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha”. (1Sam. 15:10,11)

Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, Ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli?

Nehemia

Katika Nehemia 5:14-19 tunaona Nehemia alionyesha msimamo wa haki, kama maadili yake binafsi.
- Alikusudia kufanya yaliyo mema na ya haki (mst.14)
- Alijitenga na watu walio wadharimu (anasema sikufanya kama maliwali walionitangulia. Mst. 15)
- Alijitoa na kukaza macho yake kwenye kazi (“maana hata kazi ya ukuta nikaishika sana”. Mst. 16)
- Nehemia pia alikuwa na uwezo wa kuwavuta wengine (nguvu ya ushawishi).
-- alitoa mali zake kusaidia wengine. (Mst. 17: “watu 150 walikula mezani pangu”)
-- alitanguliza maslahi ya wengine kwanza, badala ya faida yake. (Mst. 17-18)
-- Alionyesha kuwajibika kwa Mungu akimpa utukufu. (Mst. 19)
Nehemia 12:40,43: “Ndivyo walivyosimama mikutano yao walioshukuru nyumbani mwa Mungu, na mimi (Nehemia)… Wakatoa dhabihu nyingi siku ile, wakafurahi; kwa kuwa Mungu amewafurahisha furaha kuu; na wanawake pia na watoto wakafurahi, hata ikasikiwa mbali sana furaha hiyo ya Yerusalemu”.

Kukosa maadili mema kunajidhihirisha katika mambo yafuatayo :-
i). Maisha ya uasi kwa kiongozi kama vile wana wa Israeli. (1Kor. 10:1-5)
- Kutamani mabaya. (1Yoh. 2:15-17)
- Kuabudu sanamu
- Uasherati
- mawazo potofu,
- uhusiano mbaya wa mke na mume,
- kukosa hekima katika kushauri/kushauriwa.
- Kumjaribu Bwana
- Manun’guniko.

Anatazamiwa kiongozi ya kuwa “Alivyo kwa nje na ndivyo anatakiwa awe kwa ndani. Vile anavyokuwa madhabahuni/mbele ya watu ndivyo anatakiwa awe pia mbele ya familia yake”.

ii). Maisha mabaya katika fedha.
- Kupenda fedha. (1Tim. 6:6-10)
- Kutumia vibaya fedha za kanisa. (Fil. 4:11-12)
- Udanganyifu katika matumizi. (Mith. 15:27, Rum. 13:8)
- Kutokutoa fungu la kumi (zaka) na husababisha laana kwake yeye mwenyewe na kwa kundi lake. (Mal. 3:8,9, Ebr. 7:5,9,10)
- Uzembe wa kutolipa madeni. (Zab. 37:21, Mith. 22:7) hali hii inapozoeleka kwa kiongozi inamsababishia kutoaminiwa na kuonewa shaka.

iii). Matatizo katika ndoa. Yanaweza kusababishwa na
- Unafiki. Nje kuonekana tofauti na hali halisi ya ndani, kuficha au kufanya siri shida na matatizo ya kindoa. (Math. 23:27,28)
- Kutokutatua matatizo madogomadogo ya ndani, na hivyo kuzaa matatizo makubwa. (Lk. 16:10) “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia, na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia” Yapasa kujiuliza. Je, una ujasiri wa kuhubiri mbele ya mkeo au mumeo na pia watoto? Kama unakosa ujasiri mbele yao, basi, kuna mambo yanahitajika ufumbuzi.
- Kuacha kutunza familia kwa kisingizio cha kutingwa na huduma. (1Tim. 5:8)

iv). Kuharibu huduma yako kwa:-
- Kupotosha Neno la Mungu, kughoshi, na bila ya kutumia kwa halali neno la kweli. (2Kor. 4:1,2, 2:17, 2Tim. 2:15)
- Kuwatumia watu kwa kujinufaisha yeye binafsi badala ya kuwajenga na kuwaimarisha katika ufalme wa Mungu.


Faida ya Maisha ya Maadili mema ya kiroho

Ili uwe kiongozi, lazima uwe na wafuasi, kuwa na wafuasi lazima wakuamini. Hivyo maadili bora, ni ya lazima; yanakuwezesha wewe kiongozi katika mambo yafuatayo:-
- Kuirithisha (influence) tabia yako kwa wale unaowaongoza. (Mat. 26:73) ”Punde kidogo,wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe u mmoja wao, kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha” (1Tim. 4:12)
- Kutokuwa mtu wa kubadilika badilika kama kinyonga.
- Je, wewe ni yeye yule kila wakati?
- Je, jambo gani unafanya ambalo hutaki watu walijue?
- Hii ndiyo tabia yako? (1Tim. 3:8)
- Tabia yako isiyobadilika inagusa mioyo ya watu. (Ebr. 13:7)
- Dhamiria kuwa mkweli na muwazi, usitafute kuonekana mzuri, bali uwe mzuri. (Yer. 7:3-4)
- Tabia huweza kujengwa na kubomolewa katika mambo madogo. Dhamiria uaminifu katika yaliyo madogo hivyo utakuwa mwaminifu dhidi ya mambo yaliyo makubwa.
- Unaweza ukabadili matendo yako ili yafuatane na kanuni za maadili mema au unaweza ukabadili kanuni za maadili zifuatane na matendo yako. Uchaguzi ni wako!
- Dhamiria kuwa na nia ya kutumika kwa unyenyekevu, watu watakufuata wakijua nia na lengo lako ni kuwatumikia.

Changamoto
- Hitaji kubwa la kanisa ni kupata viongozi bora, watakaoweza kukabiliana na changamoto zilizopo nyakati hizi za mwisho katika kumwakilisha Kristo. Je, wewe ni miungoni mwao? (1Tim. 3:1-7)
- Utafanya nini wewe binafsi ili kuboresha uongozi wako?


6. MAFAO, GHARAMA NA ANASA ZA UONGOZI

Uongozi una mafao, gharama na anasa zake, anasa ni pamoja na vikwazo vilivyomo.

i). [a]. Mafao ya Uongozi. (1Thes. 5:12,13, Ebr. 13:17, 1Pet. 5:2-4, 1Kor. 9:10)
- Heshima katika jamii. (Social status)
- Kutambuliwa na kueleweka (recognition and position)
- Mapato. (Material gain)
- Mamlaka (Power and authourity)
- Kuwa na mvuto kwa watu (Influence on large scale)
- Mafao ya kiroho. (Spiritual benefits)

[b]. Kutawala vema mafao ya uongozi.
- Uuone uongozi kama dhamana.
- Uwe na nia ya utumishi.
- Jifunze kutofautisha kati ya mambo yako binafsi na cheo. Panga maisha ambayo unaweza kuishi bila cheo.
- Wekeza kwa ajili ya siku za mbele.
- Uwe tayari kumpisha mwingine kuchukua cheo chako, andaa viongozi.
- Mwamini Mungu katika nafasi uliyo nayo.

ii). [A]. Gharama ya Uongozi.
- Kujitoa muhanga kwa ajili ya wengine. (personal sacrifice)
- Mateso ya kibinafsi – kutokana na hisia mbalimbali.
- Kukataliwa, kukatishwa tamaa, kuchekwa na kuzomewa nk.
- Kulaumiwa
- Kudhalilishwa
- Matatizo ya ndoa na familia
- Kuingiliwa katika maisha kwa mambo binafsi
- Upweke
- Kuwa tayari kushindwa
- Kuwa tayari dhidi ya majaribu yanayotokana na fedha, zinaa na matumizi mabaya ya madaraka nk.

[B]. Kukabiliana na gharama za madaraka/uongozi.

Mjue sana Mungu na kumpenda. (Fil. 3:8-10)
- Jiandae kukabiliana na gharama hizo. (Fil. 1:27-29)
- Tumia muda wako vizuri kwa mambo yote, yaani uwe na kiasi. (Kol. 4:5, Ef. 5:15,16)
- Uwe tayari kuwajibika.
- Uwe mtu wa maombi, ili kumshirikisha Mungu mambo yote na kumtegemea. (Zab. 37:2-7,23)

iii). [a]. Anasa au Majaribu ya uongozi. (vikwazo)

Uongozi huambatana na anasa zake, ambayo ni mitego na majaribu kwa kiongozi.
Baadhi ya majaribu ni:-
- Kujiona umefika juu ya kilele (kiburi). (Isa. 14:13,14. Mithali 29:23)
- Kushindwa kuendelea kuwa na maono. (Mithali 29:18)
- Kuacha kuwa mfano wa kuigwa.
- Kutumia madaraka kwa faida binafsi.
- Kukataa kujipima mwenyewe.
- Kuridhika na utendaji usioridhisha.
- Kutumia vibaya madaraka kwa watu.
- Zinaa.
- Kujisifu na kujiinua.
- Wivu.
- Kutojali familia.
- Uvivu, kukosa motisha na kuahirisha mambo.
- Kujisikia huwezi na hufai.
- Kupoteza dira ya uzima wa milele.

[b]. Kukabiliana na anasa, mitego na majaribu ya uongozi.
(2Tim. 4:15,16, 1Thes. 4:1, 1Thes. 5:17,18, Fil. 4:6,7)

- Kukaa katika maadili mema ya kikristo
- Kudumu na kutii Neno la Mungu
- Maombi. (Mith. 16:3) “Mkabidhi Bwana kazi zako, na mawazo yako yatathibitika”.
- Kuhusisha mambo yako kwa walio karibu nawe, watu au timu yako ya uongozi kwa ushauri. (Mith. 20:18) “Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita” (Mith. 15:22)








SEHEMU IV



7. SIRI YA MAFANIKIO YA UONGOZI WA KIROHO

Pamoja na kuwa na maadili bora, mambo yafuatayo ni muhimu sana kwa kiongozi.
i. Kumwamini na kumpenda Mungu. (Yoh. 14:1, 12,21,23)
ii. Kufanya mapenzi ya ya Mungu. (Mat. 7:21, Ef. 5:10)
iii. Maombi. (Lk. 18:1, 1Tim. 2:1, Lk. 6:12, Mk. 1:35-39, Ebr. 5:7-10, Ezr. 8:21-23)
iv. Kuwa na Mipango mizuri. (Lk. 14:28-32, 1Tim. 3:15)
v. Kujali rasilimali ulizonazo, pamoja na muda. Kut. 10:25-26,8,9, Lk. 22:35,36, Ef. 5:15,16)
vi. Mahusiano bora na wengine wanaokuzunguka. (Ebr. 12:14,15, Yoh. 13:34,35)

8. MAONO NA MALENGO YA KIONGOZI

Malengo ni tofauti na Maono.

A]. Maono ni uwezo wa kupata picha ya mambo ya siku za mbele.

Ni kufanya safari toka kwa unayoyaona sasa kwa yasiofahamika na kuyaona kama yapo.

Mfano tunajifunza ya kuwa:-
- Nuhu aliona mapema gharika juu ya uso wa nchi akawaonya watu wake. (Mw. 6:13-17,22)
- Yusufu aliona miaka saba ya njaa kabla ya kutokea. (Mw. 41:28-30)
- Musa aliona nchi ya ahadi. (Kut. 3:3-9)
- Nehemia aliona Yerusalemu mpya. (Neh. 1:2-6, 2:3-5)
- Paulo aliona Makedonia inahitaji injili. (Mdo. 16:9,10)
- Nawe unaona maono gani? Juu ya kanisa na familia yako, na mengine?

B]. Baada ya kuona maono.

Ni lazima mambo yafuatayo yafanyike ili maono yawe mambo au kitu halisi na wala si ndoto za kupita tu.
- Kufanyika kazi ya kuhamasisha. Utahitaji mtu au watu katika kuyatimiza mambo uliyoyaona. Musa alihitaji kuwaona wazee wa Israeli kwanza. (Mw. 3:16-18, 4:29,31) Hivyo ivyo, Nehemia, katika sura 2:17-18 katika kitabu cha Nehemia.
- Kuweka malengo, mipango ya utekelezaji ili kuyafikia hayo maono. Pasipo malengo, na mipango mizuri watu watashindwa kuyafikia maono, na hawawezi kuhamisika kuendelea mbele kuyatekeleza. Hatimaye kila mtu atafanya anavyoona machoni pake mwenyewe. (Amu. 21:25)

C]. Msingi wa Biblia kuhusu kuweka malengo.

Yesu alitoa mfano wa mjenzi wa mnara na mfalme aendaye vitani. (Lk. 14:28-32)
Mjenzi katika kuweka malengo, inamlazimu, kuchora ramani, kukusanya vifaa, na rasilimali zingine, kisha kuanza kujenga hatua kwa hatua.
Mpiganaji, kabla ya vita hujiandaa, huandaa majeshi, vifaa, silaha na njia za kuendelea na hivyo hujipanga kikamilifu kabla yayote kwa nia ya kupigana.
Mpango wa Mungu wa wokovu ulikuwa na malengo na mipango yake ya utekelezaji.
- Mungu aliandaa Mtu mmoja, ambaye ni Ibrahimu, baba wa imani
- Taifa la Israel kuwepo
- Manabii
- Yesu kuzaliwa awe mwokozi wa ulimwengu
- Mitume
- Roho mtakatifu
- Kanisa. Hatimaye Wokovu wa milele (Uzima wa milele).

D]. Faida ya kuweka malengo na mipango.

i). Huwezesha kuwa na mwelekeo wa mambo/kazi katika maisha.

Watu wasio na malengo hawafiki popote. Malengo na mipango hufanya maisha yawe ya maana na huweka mwongozo wa maisha.
Kama hujui unakokwenda, njia yoyote itakufikisha huko usikokujua”.
Ukilenga hewa utafanikiwa kupiga shabaha hiyo, na hakuna anayelenga hewa akaikosa”.

ii). Huhamasisha mambo kufanyika.

Viongozi wengi waliofaulu wanakiri kuwa walihamasika na malengo waliyokuwa nayo, na kujiona wakitembea kuelekea katika malengo hayo. Ni malengo yanayowaelekeza ni wapi wawekeze na kutoa vipao mbele katika mali na rasilimali walizonazo na pia nguvu zao.

iii). Humfanya mtu kuwa na tabia ya kutaka kuona matokeo.

Malengo na mipango humfanya kiongozi awe na hamu ya kuona matokeo yake ya kazi anayoifanya na maendeleo yake yalivyo. Yanamfanya mtu kuweka mkazo katika matokeo, badala ya shughuli zinazofanyika. Kwa sababu hiyo pia husaidia:-
- Kupima utendaji na shughuli za kazi
- Kujua umekwenda umbali gani?
- Kuwajibika
- Kutadhimini kazi mara kwa mara na kuboresha utendaji.

Hivyo viongozi waliofaulu ni watu ambao wana malengo kwa siku za mbele. Si watu wa kushughulikia matukio tu, au watu wa mambo yaliopita. Huwa hawasubiri mambo yatokee na ndipo wafanye kitu. Ni watu wanaojitahidi kutimiza mambo kwa vile:-
- Wana maono yaliyo wazi.
- Hujiwekea mipango na ratiba ya kutimiza maono hayo.
- Wanawajibika katika kufuatilia malengo yaliyowekwa.
- Huvumilia wakati maono, malengo, na mipango. Hukutana na vikwazo mbalimbali, na kutotimizwa waliyoyakusudia kwa wakati uliokusudiwa.
- Hutafuta ufumbuzi na kubuni njia ya kuendelea mbele si kurudi nyuma na kukata tamaa.

Kuna viongozi wa aina mbili. Wale wanaosababisha mambo kutokea, na wale wanaosubiri mambo yatokee.

i. Viongozi wanaosababisha mambo yatokee
wana mtazamo wa mbele
wako tayari kupanga mipango, kuona jinsi gani watayatimiza hayo maono yaliyopo.
Wanaweka mikakati ya kuzuia matatizo yatakayoweza kutokea.

ii. Viongozi wanaosubiri mambo yatokee.
hawafanyi chochote , bali wanasubiri mambo yatokee, ndipo wajishughulishe
hutumia muda mwingi kushughulikia matukio.
Ni wazima moto na kutumia muda mwingi kuzima moto kiasi cha kufanya hata wasiweze kujiuliza kwa nini moto unatokea?

Tofauti kubwa kati ya viongozi wa aina hii ni uwezo katika kuweka malengo na kujishughulisha na mipango pia mikakati mbalimbali katika kutimiza maono yaliopo.

Maono, malengo na mipango lazima yawe SMART. Yaani sifa zenye:-
-- Spirit led and Specific - Uongozi wa Roho na yenye shabaha.
-- Measurable - kunapimika
-- Attainable - kufikika
-- Realistic - halisi
-- Time targeted - muda maalum.

Maono yanaweza kushindikana kufiwa kutokana na kuwa, hayakuwa na shabaha maalum, wala hayapimiki, tena sio rahisi kufikika na huenda sio halisi kibinadamu. Labda hayakutengewa muda maalum, yangekuwa na muda yangeweza kuhimizwa na kukamilishwa haraka na hivyo kufurahia matokeo yake. Mawazo (maono) yako yafafanuliwe kwa maneno yako, maneno yazae matendo na tabia (malengo, mipango na mikakati). Hatimaye yataoneka Matokeo kamili (kitu halisi) kutokana na mawazo uliokuwa nayo. Bila kujitahidi kufanya hivyo, mawazo au maono yako yatakuwa sawa na ndoto za mchana, yasiyoweza kufikiwa au kutekelezeka kamwe na mtu yeyote.

Hivyo basi kiongozi wa kiroho huwa na mtazamo wa kimungu. Kama vile Mungu Mwenyenzi alivyo na maono thabiti tangu mwanzo hadi mwisho wa kazi zake katika ulimwengu huu na ujao. Mipango yake katika mikakati ya wokovu imekuwa na ushirikishwaji wa mwanadamu na kwa uwazi kabisa.

Rumi. 8:28: ”Nasi tunajua ya kuwa katika mabo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake”. Yeye ni Mungu anayeenda kwa muda na majira alioyakusudia tangu Adamu kuumbwa hadi Yesu Kristo na hata mwisho wa dunia na hukumu ya ulimwengu. Kazi na matukio tunayoyaona ni yale yaliyotabiriwa na manabii tangu hapo awali. Kwa hiyo Uongozi wa kiroho unabeba sura ya Mungu mwenyewe kwa wana wa Mungu wanaomtegemea.

Biblia inasema hivi:
- Mith. 16:4: “Mkabidhi Bwana kazi zako na mawazo yako yatathibitika.”
- Rumi. 8:14: “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndio wana wa Mungu.”
- Yoh. 15:6: “Akaaye ndani yangu (Yesu) nami ndani yake huyo huzaa sana; pasipo mimi (Yesu) ninyi hamuwezi kufanya neno lolote.”
- Isaya 14:24: “Bwana wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile nilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa, na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea.
- Math. 28:20: “…Tazama, nipo pamoja nanyi siku zote hata ukamilifu wa dahari.”


Amina




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni